Tabora. Siku moja baada ya kutokea kwa ajali ya basi la Happy Nation iliyotokea katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na kusababisha kifo cha mtoto mmoja, tayari mtoto huyo, Yumwema Charles (4) ametambuliwa na ndugu zake.
Ajali hiyo ilitokea Julai 17, 2024 alfajiri baada ya basi hilo kuligonga lori linalomilikiwa na Kampuni ya Dangote lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara katika Kata ya Pangale wilayani Sikonge na kusababisha kifo cha mtu huyo na kujeruhi wengine 19.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoani humo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi ambaye aliendesha bila kuchukua tahadhari za usalama barabarani na hadi sasa anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo.
Akizungumzia na Mwananchi leo Julai 18, 2024 kuhusu maiti hiyo iliyohifadhiwa kwenye hospitali yake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Dk Patrick Bilikundi amesema aliyefariki kwenye ajali hiyo ametambuliwa na ndugu zake.
“Baada ya ajali kutokea, tukaanza jitihada za kuona namna ndugu wa marehemu Yumwema Charles (4) wanavyoweza kupatikana, kwa hivyo jioni tulipata mawasiliano ya ndugu ambao makazi yao ni Katavi, wameshafika hapa hospitali na wameutambua mwili wa ndugu yao na tumesharuhusu mwili kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Katavi kwa mazishi,” amesema.
Ameongeza kuwa katika majeruhi 19 waliofikishwa hospitalini hapo jana Julai 17, 15 miongoni mwao waliruhusiwa kuendelea na safari zao baada ya kupewa huduma ya kwanza na hali zao zinaendelea vizuri.
Bilikundi amesema majeruhi wawili kati ya watatu waliopata majeraha makubwa baada ya ajali hiyo, wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
“Tuna majeruhi wawili ambao walipata mivunjiko ya miguu na sehemu za nyonga, tumewapa rufaa kwenda hospitali ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi kwa kuwa kesi zao hapa hospitali tusingeweza kuwatibu inavyotakiwa na hadi sasa tumebaki na mgonjwa mmoja ambaye alifanyiwa upasuaji wa miguu na anaendelea kupatiwa matibabu,” amesema.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Tabora Costantine Mbogandi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.