MLEZI na mshauri mkuu wa Pamba Jiji, Said Mtanda amesema jumla kuu ya bajeti ya uendeshaji wa timu hiyo msimu huu katika ushiriki wake Ligi Kuu ni takribani Sh1.5 bilioni, huku ikitumia zaidi ya Sh300 milioni kwenye usajili wa dirisha kubwa.
Timu hiyo itacheza Ligi Kuu Bara inayoanza Agosti 16, mwaka huu baada ya miaka 23, huku ikileta benchi jipya la ufundi likiongozwa na Goran Kopunovic, Salvatory Edward na Razack Siwa, huku ikisajili nyota wapya 17 na kuwaongezea mikataba saba.
Akizungumza baada ya kupokea Sh10 milioni kutoka kwa Mhuburi wa kimataifa kutoka Kenya, Ezekiel Odero, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema katika bajeti hiyo wanahitaji Sh450 milioni za kununua basi la timu na tayari wameshakusanya Sh200 milioni.
“Tumetumia takribani Sh300 milioni katika usajili kuhakikisha tunakuwa na timu bora na mwezi wa nane tutafanya tamasha kubwa, tumeomba baadhi ya viongozi wizarani watufanyie hamasa kwa wadau tuweze kununua basi linalogharimu Sh450 milioni.”
“Sisi tumeshapata Sh200 milioni na tunaendelea kuhamasisha. Tumepata wadau wametudhamini Sh400 kwa hiyo jumla kuu ya uendeshaji wa timu ni zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa msimu, hivyo, kwa mchango huu naamini utafungua njia kwa wadau wengine,” alisema Mtanda
Mhuburi Ezekiel Odero akizungumza baada ya kukabidhi Sh10 milioni, ahadi ya jezi jozi mbili na mipira mitatu kwa timu ya Pamba Jiji, alisema huo ni mwanzo kwani baada ya kukamilisha tamasha lake lake jijini hapa ataongeza msaada kwa timu hiyo.