NEW YORK, MAREKANI: MAURICIO Pochettino ameripotiwa kujitokeza kama mtu anayepewa nafasi kubwa ya kupewa kiti cha ukocha wa timu ya taifa ya soka ya Marekani baada ya kutimuliwa kwa Gregg Berhalter.
Berhalter alifutwa kazi baada ya matokeo mabovu ya kikosi cha Marekani kwenye michuano ya Copa America 2024 ambako walitolewa katika hatua ya makundi. Katika kutafuta kocha mpya, iliripotiwa kuwa chama cha soka cha Marekani (US FA) kiliwasiliana na kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp ili akachukue mikoba hiyo. Hata hivyo, baada ya
Klopp kukataa ofa hiyo, macho yao sasa yameelekezwa kwa Pochettino, kwa mujibu wa Diario Ole.
Pochettino hana ajira hivi sasa baada ya kufutwa kazi na Chelsea mwezi Mei baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya sita ya Ligi Kuu England.
Wasifu wake unaendana na kile ambacho Marekani inakitafuta: kocha kijana mwenye rekodi nzuri, anayezungumza Kiingereza fasaha, na ambaye amefundisha soka la daraja la juu katika ligi kubwa.
Pochettino, 52, amefanya kazi katika soka la ushindani akifundisha Tottenham Hotspur, ambako aliiongoza timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na Paris Saint-Germain (PSG).
Ofa ya Marekani inaweza kumvutia kwa sababu atapata fursa ya kuviunga pamoja vipaji vya wachezaji vijana wa Kimarekani kama Gio Reyna, Folarin Balogun na wengineo katika staili na falsafa yake anayoipenda ya kutembeza boli.
Kama Pochettino atachukua ofa hiyo kutoka US FA, atapata nafasi ya kuiongoza timu katika fainali za Kombe la Dunia 2026 mbele ya mashabiki wao katika viwanja vya nyumbani kama wenyeji pacha wa michuano hiyo. Hii inaweza kumvutia kocha huyo Muargentina kuchangamkia fursa ya kumfundisha Christian Pulisic na wenzake.