Polisi yapokea vibanda maalumu kuboresha usalama barabarani

Dar es Salaam. Katika kuimarisha usalama barabarani, Kampuni ya Bima ya Milembe imekabidhi vibanda vitano maalumu vilivyoundwa kwa ajili ya askari wa usalama barabarani wa Jeshi la Polisi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Bima ya Milembe, Muganyizi Tibaijuka amesisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha usalama barabarani.

“Tunatambua umuhimu wa jitihada endelevu za Serikali katika kuboresha usalama barabarani. Kufikia malengo haya kunahitaji washikadau wa usalama barabarani kushirikiana bega kwa bega, ndiyo maana tunatoa vibanda hivi,” amesema Tibaijuka.

Amesema ushirikiano huo unaashiria hatua kubwa katika kuimarisha usalama barabarani jijini Dar es Salaam na kuonyesha mchango mkubwa wa mashirika ya kibiashara katika kusaidia mipango ya serikali kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Solomon Mwangamilo ametoa shukrani kwa niaba ya Jeshi la Polisi.

“Tunashukuru kupokea vibanda hivi kwani vitaongeza ufanisi wa kuratibu usalama barabarani. Tutaendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika,” amesema Mwangamilo.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Hadija Maulid ameipongeza Kampuni ya Bima ya Milembe kwa umakini wake.

“Bima ni mdau mkubwa wa usalama barabarani na ushirikiano huu unaendana na mikakati ya TIRA ya kukuza elimu ya bima na umuhimu wake ndani ya jamii,” amesisitiza.

Related Posts