Serikali yasema elimu ya bidhaa bandia itolewe kuanzia ngazi ya mitaa

Dar es Salaam. Serikali imewataka wazalishaji nchini kuendelea kutoa elimu ya bidhaa bandia hadi ngazi ya mitaa kwa kuwa huko ndiko walaji wengi wapo.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Julai 18, 2024  na  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe  kwenye maadhimisho ya kitaifa ya kudhibibiti bidhaa bandia duniani aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kigahe amesema walaji wakipewa elimu sio tu watasaidia mapambano dhidi ya bidhaa bandia bali watachangia bidhaa za wazalishaji kujulikana kwa wanunuaji.

“Bidhaa bandia zimekuwa zikididimiza uchumi, wazalishaji kupata hasara, lakini kuweka rehani maisha ya watumiaji, hivyo kutoa elimu kutawasaidia mambo mengi na kukuza uchumi wa nchi na kuwa na biashara shindani,” amesema.

Pia, amesema kwa upande wa Serikali  pamoja na jitihada mbalimbali inazozichukua pia kuna mpango wa kurekebisha sheria zilizopo katika kukabiliana na bidhaa hizo ili ziendane na wakati wa sasa wa sayansi na teknolojia.

Kigahe amesema sheria zinazotumika ni za tangu mwaka 1963, hivyo kushindwa kukabiliana na njia nyingine mpya ambazo wanaoingiza bidhaa hizo wamekuwa wakizitumia.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio  amesema maadhimisho hayo yalianza tangu Julai 14 2024 na kumekuwa na shughuli mbalimbali ikiwamo utoaji elimu mtaani, kufanyika maonyesho na leo ndio kilele.

Pia, amesema kumefanyika kongamano la kutafuta namna bora za kukabiliana na bidhaa hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameahidi wawekezaji wa ndani na wa nje kutengenezewa mazingira bora ya kupambana na bidhaa bandia.

“Serikali inafanya hivyo ikitambua kuwa mkoa huu ndio lango kuu biashara, wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiutumia kama mwanya  katika  kuingiza  bidhaa nyingi bandia ukilinganisha na mikoa mingine,” amesema Bomboko.

Kwa upande wao wazalishaji akiwamo ofisa masoko kutoka kampuni ya kuuza tela na vipuri vya magari ya Superdoll, Dominic Chuwa amesema bado kuna changamoto katika udhibiti wa bidhaa hizo ikiwamo kuwajua wazalishaji wake wakubwa.

“Kisheria huwezi kwenda kumshitaki muuzaji mdogo, lazima umpate yule papa mwenyewe na kwa bahati mbaya hawa wapo nje ya nchi, hivyo inakuwa ngumu kuwakamata kirahisi,” amesema Chuwa.

Evanice John, ofisa msaidizi kutoka kampuni ya dawa za meno ya Colgate Palmolive, amesema kinachowaponza wananchi ni kununua bidhaa bandia kwa kuangalia urahisi wa bei bila kuangalia ubora wake.

“Kwa mfano sisi mswaki wetu tunauza kati ya Sh2,000 hadi Sh2,500 lakini ukienda Kariakoo miswaki hiyo hiyo unakuta inauzwa mitatu Sh1,000 na kujikuta wengi wakiikimbilia,”amesema Evanice.

Related Posts