Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amependekeza kuwapo kwa mpango mkakati wa miaka mitano wa ukusanyaji kodi ili kujua kama nchi itapata wapi kodi badala ya kusubiri miezi michache kabla ya bajeti.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Julai 18, 2024 wakati akiwasilisha maoni yake katika kikao kilichofanyika baina ya viongozi mbalimbali wa taasisi za sekta binafsi, viongozi wa vyama vya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kikao hicho kinafanyika ili kusikiliza changamoto zilizopo katika ufanyaji wa biashara Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alipokuwa akimuapisha Julai 3, 2024 kuongoza nafasi hiyo.
Baada ya kumuapisha Rais Samia alimtaka Mwenda kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi ili kuweka mazingira sawa ya biashara.
Akizungumza katika kikao hicho, Ngalula amesema kama nchi mara zote imekuwa ikifahamu mwaka unaofuata kuna bajeti inayopaswa kupitishwa hivyo ni vyema kuwapo kwa maandalizi badala ya kusubiri miezi michache kabla ya bajeti kufika.
Amesema kutokuwapo kwa maandalizi ndiyo kunasababisha matumizi ya kikosi kazi katika ukusanyaji mapato ambayo mara zote imekuwa ikisababisha kelele kwa wafanyabiashara.
Pia, amesema kukosekana kwa mpango huo ndiyo unasababisha kodi kuendelea kuongezwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo vinywaji.
“Tuwe na mkakati kuangalia kodi yetu itatoka wapi inaamana kodi ya mwaka 2028 tunaanza kuijadili leo lakini kama tutakuwa tunakaa tunasubiri imebaki miezi michache bajeti ya mwaka 2025/2026 tunasubiri Desemba ndiyo tunaanza kuitana kwenye kikosi kazi kujadili kodi inapatikana wapi mwisho wa siku tunaishia kurudisha mlemle,” amesema Ngalula.
Ametaka kuwapo kwa watu wanaofikiri nje ya boksi ambao si lazima wawe wasomi tu na badala yake wawepo na wafanyabiashara wanaoweza kuonyesha kodi hiyo inakoweza kupatikana.
Amesema kwa sasa watu wengi hawalipi kodi huku akisema wapo hadi machawa wanaofanya ujasiriamalu ambao wanaingiza fedha nyingi lakini hawalipi kodi.
“Wale wanafanya utangazaji wa bidhaa mnaweza kuweka mfumo walipe kodi kwa sababu wanapata fedha, tuangalie maeneo ambayo tunaweza kukusanya kodi lakini hayajaguswa na yakaingiza mapato mengi, kuna sehemu kama ufugaji na hata bodaboda kwani wapo wenye uwezo wa kulipa,” amesema Ngalula.
Namna nyingine ya kuweka uhakika wa kupatikana kwa kodi hiyo ni kupanua wigo wa walipakodi kutoka zaidi Sh2 milioni kwa sasa kati ya watu milioni 61.
Katika kuongeza wigo wa walipakodi, ametaka kuwekwa urahisi na motisha ili watu waweze kurasimisha biashara zao na kuanza kulipa kodi.
“Mimi ni mama ntilie nafanya biashara chini ya mwembe sina tozo za OSHA, TBS, sina mtu wa afya atakayenisumbua lakini nimejikusanya nifungue kaofisi kadogo asubuhi TRA ameshafika mlangoni. Mtu akiwa ana bodaboda nyingi hahitaji leseni lakini nikisema nafungua kampuni ni kosa la jinai,” amesema Ngalula.
Amesema ni vyema kama nchi ikawa tayari kwenda nje ya mipaka kuangalia na kujifunza washindani wao wanafanya nini ili vije vitekelezwe nchini.
Ametumia nafasi hiyo kuzungumzia suala la baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu ambao alieleze wamekuwa wakivuka mstari katika kutekeleza majukumu yao.
“Sheria zipo na zimewekwa tuko tayari kuzifuata baadhi ya wachache kwenye kutekeleza majukumu yao wanauvuka kuingia mstari mwingine na matatizo yapo sehemu ambazo zinazungumzika,” amesema Ngalula.