Lindi. Ili kupanua wigo na upatikanaji wa Elimu ya juu nchini hususani taaluma ya kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Saaam (Udsm) kimeamua kujenga matawi mkoani Lindi kwa ajili ya Kilimo.
Kimesema tawi moja litatumika kama kituo cha utafiti wilayani Ruangwa katika Kijiji cha Likunja huku tawi lingine likijengwa Manispaa ya Lindi katika eneo la Ngongo kwa ajili ya masomo hayo ya kilimo.
Naibu makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dar es salaam (Mipango, Fedha na Utawala) ambaye ni mratibu wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi (HEET) chuoni hapo, Profesa Bernadeta Killian.
Akizungumza wakati wa kutambulisha kamati ya kupokea maoni na malalamiko kuhusu mradi leo Alhamisi Julai 18, 2024, Profesa Killian amesema wameamua kujenga matawi mawili mkoani Lindi kwa kuwa mkoa huo unajishughulisha na kilimo na ni mkoa unaotoa mazao mengi.
Profesa Kiliani amesema watahakikisha ujenzi wa kituo cha utafiti wa sayansi ya kilimo na chakula cha Udsm unaofanyika katika Kijiji cha Likunja wilayani Ruangwa, unakamilika ndani ya miezi 18, huku chuo kinachojengwa wilayani Lindi, ujenzi wake umeshaanza katika eneo la Ngongo.
“Tumeamua kujenga mkoani hapa kwa kuwa ni moja ya mikoa inayotoa mazao mengi na ni mkoa ambao unajishughulisha na kilimo kwa asilimia kubwa,” amesema Profesa Killian.
Profesa huyo amesema ina jukumu la kukusanya malalamiko kutoka kwa wananchi kwa lengo la kuboresha hususan mahali mradi unapojengwa sambamba na kuweka kumbukumbu ya kile kinachoendelea na kufanyika katika mradi.
Naibu mratibu wa mradi huo wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi (HEET), Dk Liberato Haule amesema mradi huo unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa udhamini wa Serikali kupitia fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia ukilenga kuboresha huduma za elimu ya juu nchini ili iweze kuchangia maendeleo ya uchumi kama ilivyokusudiwa.
“Mradi huu unatekelezwa katika maeneo mapya 14 ambapo mpaka sasa maeneo mapya matatu tayari yameshafikiwa ambayo ni pamoja na Ngongo (Manispaa ya Lindi), Likunja wilayani Ruangwa pamoja na Kagera,” amesema Haule.
Bakari Juma ni mjumbe wa kamati ya Kasema kutoka Wilaya ya Ruangwa, amesema wana matumaini makubwa na mradi huo na kukamilika kwa kituo hicho kitakuwa msaada kwa wakulima na kitasaidia kuongeza fursa za kiuchumi.
“Chuo hiki kikijengwa kitawasaidia hata watoto wetu ambao watataka kujifunza na hata baadhi ya wakulima ambao pia watakuja kujifunza mambo mbalimbali ya kilimo,” amesema Juma.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ameitaka kamati ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tawi la Lindi kinachojengwa katika eneo la Ngongo Manispaa ya Lindi, kufanya kazi kwa uweledi na uzalendo kwa maslahi ya mkoa na Taifa kwa ujumla.