Dar es Salaam. Wakati kelele nyingi za ukatili dhidi ya wanawake zimekuwa zikielekezwa kwa wanaume, utafiti umebaini wanawake kwa wanawake pia hufanyiana ukatili kwa kuendeleza mila na desturi potofu.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vinavyofanywa na wenyewe kwa wenyewe havichukuliwi uzito, kwa kile kinachoaminika ni kuendeleza mila na tamaduni za jamii husika.
Utafiti huo uliofanyika katika mikoa ya kanda ya ziwa umeonyesha bado kuna mila na desturi potofu, ambazo zinaendelezwa na wanawake na kuwa mwiba kwao wenyewe.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo leo Alhamisi, Julai 18, 2024 jijini Dar es Salaam, mtafiti aliyefanya utafiti huo kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Regina Opoku, amesema licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake bado kundi hilo linaendelea kuwa hatarini kibaya zaidi ukatili huo kuendelezwa na wanawake wenzao.
“Tunapozungumzia ukeketaji mila hii potofu inapewa msukumo na wanawake, unakuta bibi, shangazi au mama anamlazimisha binti yake akaketwe ili awe mwanamke kamili, kinyume na hapo anamwambia hawezi kupata mwanaume wa kumuoa.”
“Kule Mara kuna mila ya ‘Nyumba Ntobhu’ nilipokwenda kuzungumza na wale wasichana ambao wanaolewa kwenye hizo jamii wanaeleza namna wanavyofanyiwa ukatili na hao wanawake ambao wanawachukua kama wake,” amesema Dk Regina.
Mtafiti huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu amesema tofauti na inavyoelezwa na wanawake wa jamii hiyo kuhusu Nyumba Ntobhu, mabinti wanaoingia kwenye hizo familia wanatumikishwa na kufanyiwa ukatili wa kimwili.
“Wakienda kuolewa kwenye hizo familia kazi yao ni kuzaa, kuzalisha mali na wakati mwingine wanapigwa hata kunyimwa chakula na vitendo hivi vinafanywa na wanawake wanaowalipia mahari.”
“Ukiachana na hilo kuna mila ya kutakasa, mwanamke akifiwa na mume wake anatakiwa kushiriki ngono na mwanaume mwingine kwenye familia ya mumewe kwa kile kinachoelezwa kusafishwa, hili pia linasimamiwa kikamilifu na wanawake,” amesema.
Kutokana na hilo, Dk Regina kupitia utafiti huo amependekeza Serikali kuongeza nguvu katika kuhakikisha maofisa ustawi wa jamii wanashuka zaidi kwenye jamii za aina hiyo ili kuelimisha dhidi ya vitendo vya ukatili.
Mbali na hilo amependekeza pia mfumo wa elimu kuruhusu wanafunzi wafundishwe kuzikataa mila na desturi potofu, ili wasiangukie kwenye ukatili huo unaoishia kuhatarisha afya za wanawake na wasichana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha utafiti huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema utafiti huo umeikumbusha Serikali kuwa bado kuna kazi ya kufanya katika kukabiliana na mila kandamizi.
Amesema kwa muda mrefu nguvu kubwa imeweka katika kumkomboa mwanamke kiuchumi lakini utafiti huo umeonyesha hilo haliwezi kufanikiwa kama ukombozi wa kifikra haujafanikiwa.
“Zipo mila na tamaduni ambazo zinafanya wanawake kwa wanawake kufanyiana ukatili na kurithisha vizazi na vizazi, eneo hili huenda halikufanyiwa kazi kikamilifu, hii taarifa ya kitafiti inatupa picha halisi ya mambo yanavyoendelea.”
“Tunapambana mwanamke apande ukombozi wa kiuchumi lakini kumbe wao kuna mambo yao wanayoyaendeleza na kujikuta wanarudisha nyuma kimaendeleo, kujiathiri kiafya na wakati mwingine hata kusababisha ulemavu,” amesema Dk Dorothy.
Waziri huyo amebainisha kuwa wizara yake imeanza kuzifanyia kazi tafiti zinazofanywa katika eneo la jinsia na itakaa chini na mtafiti huyo pamoja na timu yake kuuchambua ili waone mahali pa kuanzia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema wakati umefika kwa Serikali na wasimamizi wa sheria kuhakikisha wanakabiliana na mila zinazorudisha nyuma ushiriki wa wanawake na kuwapa nguvu ya kufanya uamuzi unaohusiana na maisha yao.