Wajasiriamali wapewa mbinu kulikamata soko la ngozi kimataifa

Dar es Salaam. Wajasiriamali nchini Tanzania wamepewa mbinu za kukabiliana na changamoto ya bidhaa za ngozi na vifungashio katika ushindani wa soko la kitaifa, kikanda na kimataifa.

Wajasiriamali 50 wamepewa mbinu hizo leo Alhamisi Julai 18, 2024 katika kongamano la kuwaongezea uwezo ili kuweza kushindana kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, lililoandaliwa na Jukwaa la Ubora Tanzania (NQAT) kwa kushirikiana na International Trade Center lililofanyika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo, wajasiriamali hao wameelezwa namna ya kukabilia na changamoto za ushindani na kutumia fursa zilizopo katika masoko hayo sanjari na kuwa na mbinu zitakazowaimarisha sokoni.

Mjumbe wa NQAT, Suleiman Abdalla amesema kongamano hilo limeangazia bidhaa tano.

Amezitaja bidhaa hizo ni ngozi, kahawa, parachichi, viungo na bidhaa za vifungashio ambayo NQAT wameichukua kama sekta kutokana na kuwepo kwa changamoto kwenye eneo la vifungashio.

“Kifungashio ndio sura ya bidhaa, ingawa kuna changamoto kwenye ubunifu, wabunifu wengi nchini hawajabobea kwenye eneo hilo hivyo kushindwa kuelewa ni kwa namna gani vile vinavyozalishwa vitakidhi ubora,” amesema.

Amesema, changamoto nyingine kwenye vifungashio ni upatikanaji wake hasa kwa wajasiriamali kwani mahitaji na kilichopo sokoni ni tofauti.

Akizungumzia bidhaa ya ngozi, amesema huko kuna fursa pia japo wajasiriamali wengi hawajafahamu namna ya kuitumia ipasavyo.

“Tanzania ina mifugo mingi, lakini kwa ukanda wetu tukiangalia nchi zinazozalisha bidhaa za ngozi sisi hatupo, hii inachangizwa na mambo mengi.

“Kwanza ni ubora wa kuweza kuzalisha bidhaa hizo na mazingira ya uzalishaji kutokuwa rafiki mfano ukichukua kiatu kutoka China ni rahisi kukinunua kuliko kinachozalishwa nchini, hii inatokana na masuala ya kisera,” amesema.

Amesema kinachotakiwa ni kusaidia viwanda vya ndani viweze kuhimili ushindani ambao utawasaidia wajasiriamali hao kupambana kwenye masoko hayo.

“Pia tunaangazia namna bora ya kupunguza gharama za uzalishaji ili mjasiriamali huyu asipate hasara,” amesema.

Mmoja wa washiriki, Amir Esmail amesema kongamano hilo linawajenga kumudu ushindani uliopo sokoni.

“Nchi imefunguka na kuna mikataba ya kibiashara kutoka nchi mbalimbali na ushindani nao umeongezeka.

“Pia mara kwa mara sheria mpya zinaletwa kulingana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tunatakiwa kujipanga ili isije kufika mahali tukashindwa kumudu ushindani katika soko,” amesema.

Ametolea mfano kwenye kahawa, eneo ambalo yeye anajishughulisha nalo kama mkurugenzi wa kampuni inayodhalisha kahawa ya Amimza, anasema sheria mpya itakayoanza Januari 2025 haitaruhusu kuuza kwenye soko la Ulaya kahawa iliyolimwa eneo ambalo miti imekatwa.

“Hii sheria imewekwa ili kulinda mazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuitesa dunia, ukipeleka kahawa kule utapaswa uthibitishe imelimwa kwenye eneo ambalo miti haijakatwa kwanza ndipo kahawa ikalimwa, hii ni kwenye bidhaa moja, lakini kuna bidhaa nyingi,” amesema.

Amesema hilo ni jambo ambalo Wajasiriamali wanapaswa kukumbushwa katika makongamano kama hayo ili kuendana na dunia inavyokwenda na kuepuka hasara.

Amegusia pia namna ya kudhibiti gharama za uzalishaji ili zisiwe kubwa ili kumudu kushindana kwenye bei sokoni wakizingatia ubora wa bidhaa na mjasiriamali kutopata hasara.

Related Posts