Yanga, Simba Kwa Mkapa, Azam yapelekwa Zenji

ILE Dabi ya Kariakoo ya kwanza kwa msimu mpya sasa imefahamika itapigwa Kwa Mkapa siku ya Agosti 8, ikiwa ni mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2024-2024, huku pambano jingine la michuano hiyo kati ya Coastal Union na Azam likipelekewa visiwani Zanzibar.

Simba ndio watetezi wa michuano hiyo baada ya msimu uloipita kuifunga Yanga kwa penalti 3-1 baada ya kushindwa kufungana katika muda wa kawaida katika mechi kali iliyopigwa Agosti 13 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema leo asubuhi ni kwamba mechi hizo za nusu fainali ya Ngao ya Jamii zitapigwa kwenye viwanja viwili, Simba na Yanga zitaumana Kwa Mkapa, huku Azam na Coastal zikipelekwa New Amaan Complex, Zanzibar ikiwa mechi ya kwanza ya Ngao ya Bara kuchezwa visiwani humo.

Hii itakuwa ni mara ya pili mfululizo kwa mechi za mashindano ya Bara kupelekwa Amaan, baada ya awali mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kati ya Yanga na Azam ilipigwa huko na vijana wa Jangwani kushindwa kwa penalti.
Simba na Yanga zitakutana Kwa Mkapa zote zikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita baina yao ambapo Mnyama aliendeleza unyonge kwa kufungwa mabao 2-1 baada ya awali kuchezea mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa Novemba 5 mwaka jana.

Hata hivyo, Simba inajivunia rekodi ya Ngao ya msimu uliopita ambapo iliifunga Yanga kwa penalti 3-1, huku kipa Ally Salim aligeuka shujaa kwa kudaka mikwaju ya Khalid Aucho, Zouzoua Pacome na Kouassi Yao, japo aliruhusu moja ya Stephane Aziz KI, ilihali Djigui Diarra akidaka moja ya Saidi Ntibazonkiza.

Awamu, hii timu hizo zinakutana tena katika hatua ya nusu fainali kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo itakuwa ni mechi ya kisasi na inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo ambazo kwa sasa wanatambiana aina ya mastaa wapya waliiongezwa katika vikosi hivyo.

Simba ndio yenye mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao, huku baadhi ya waliokuwa mastaa wake kama Jean Baleke na Clatous Chama wapo upande wa mtani wake Yanga, hivyo zitakapokutana utakuwa mchezo wa kuvutia. Simba imesajili sura 13 mpya, wakiwamo saba wa kigeni na sita wazawa wanaounda na wengine waliokuwepo katika pambano la msimu uliopita lililopigwa Mkwakwani, Tanga.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo washindi wa mechi hizo za nusu fainali, wataenda kukutana katika fainali itakayopigwa Kwa Mkapa siku ya Agosti 11 na siku tano baadae Ligi Kuu Bara itaanza rasmi ikishirikisha klabu 16 zikiwamo Pamba Jiji na KenGold zilizopanda daraja kutoka Ligi ya Championship.

WADAU
Staa wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garrincha’ amesema japo timu hiyo, imesajili vizuri, hapendezewi kuona mshambuliaji kama Baleke anakuwa upande wa upinzani.

“Silaha inapokwenda kwa mpinzani, maana yake unajiongezea ugumu wa vita, ingawa katika usajili uliofanywa nayaona malengo makubwa ya Simba msimu ujao na mingine mbele,” alisema nyota huyo wa kimataifa aliyewahi kuwika pia na Majimaji na Taifa Stars.

Kwa upande kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule amesema; “Itakuwa mechi ngumu, kwani timu hizo zimefanya maboresho ya vikosi vyao.”

Beki mwingine wa zamani wa klabu hizo, Amiri Maftah amesema; “Simba na Yanga hazina shoo ndogo, najua utakuwa mchezo mgumu yoyote anaweza akatoka na ushindi bila kujali nani yupo vizuri ama vibaya.”

Related Posts