Bidhaa zashuka bei, wachumi watoa somo

Dar es Salaam. Bei za bidhaa mbalimbali katika masoko kadhaa jijini Dar es Salaam zimeshuka, sababu kubwa ikielezwa ni kutokana na kuanza msimu wa mavuno.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wamesema watu watarajie bei hiyo haitadumu muda mrefu sokoni kwa kuwa ndipo wafanyabiashara wakubwa hununua kwa wingi na kuhifadhi kwenye maghala, ili kuja kuuza kwa bei kubwa baadaye.

Sababu nyingine ya bei kushuka inaelezwa ni kumalizika msimu wa mvua za masika, hivyo barabara nyingi mikoani zinapitika na kuchangia gharama ya usafirishaji mazao kutoka shambani kwenda sokoni kupungua.

Katika masoko mengi, inaelezwa bei zilianza kupungua kuanzia mwishoni mwa Aprili, hali ikitarajiwa kuendelea kuwa hivyo hadi Septemba.

Miongoni mwa bidhaa zilizoshuka bei ni vitunguu maji. Enock Kimwayeya, mfanyabiashara katika Soko la Mabibo anasema gunia lililokuwa likiuzwa kati ya Sh500,000 na Sh450,000 sasa linauzwa Sh200,000 hadi Sh180,000,

Kutokana na hilo, kilo moja ya kitunguu iliyokuwa ikiuzwa hadi Sh7,000, sasa inauzwa ni kati ya Sh1,500 na Sh1,300.

Kwa upande wa viazi mviringo (mbatata), vilivyokuwa vikiuzwa sokoni hapo Sh80,000 hadi Sh85,000 kwa gunia, sasa vinauzwa kati ya Sh75,000 na Sh70,000.

Kwa wanaonunua kwa ndoo, iliyokuwa ikiuzwa Sh20,000 hadi Sh25,000 sasa inauzwa kati ya Sh17,000 na Sh16,000.

Hata hivyo, Kimwayeya anasema kushuka kwa bei ya viazi hivyo siyo kutokana na wingi sokoni hapo, bali wanachokiona ni hali mbaya za kiuchumi kwa wananchi.

“Zamani wakati viazi bei ikiwa juu, magari ya viazi yalikuwa yamepanga foleni kusubiri wateja, hivi sasa pamoja na kushuka bei magari ni machache yanayofika sokoni kuleta bidhaa hiyo,” amesema.

Hali kama hiyo imejitokeza pia kwa ndizi, ikielezwa msimu wa baridi huwa adimu sokoni, lakini kwa sasa zimejaa na hakuna wanunuzi.

Aboubakar Juma, mfanyabiashara wa ndizi sokoni hapo, anasema mkungu mdogo wa ndizi kutoka Bukoba, mkoani Kagera unauzwa kati ya Sh45,000 na Sh25,000, ambao awali uliuzwa kati ya Sh60,000 na Sh55,000.

Kwa ndizi mshare kutoka mkoani Kilimanjaro, mkungu unauzwa kati ya Sh20,000 na Sh15,000, huku ndizi kutoka Mbeya zikiuzwa kati ya Sh35,000 na Sh20,000, tofauti na bei ya awali ya Sh40,000 hadi Sh30,000.

Masoud Fahamu, mchuuzi wa mbogamboga za jumla sokoni Mabibo, anasema gunia la hoho lililokuwa likiuzwa Sh240,000, lakini sasa ni kati ya Sh140,000 na Sh110,000.

Kiroba cha karoti cha kilo 50 kilichouzwa Sh90,000 hadi  Sh70,000 sasa ni kati ya Sh45,000 na Sh40,000. Kilo moja ikiuzwa Sh1,500 hadi Sh1,200 tofauti na Sh3,000 hadi Sh3,500 za awali.

Adam Shomari, mfayabiashara wa nyanya kwa bei ya jumla, anasema sanduku linauzwa kati ya Sh25,00 na Sh15,000, tofauti na Sh60,000 hadi Sh70,000 za awali kuanzia Oktoba, 2023 hadi Aprili, mwaka huu.

Erasto Kiria, mfanyabiashara sokoni Ilala, amesema sado ya nyanya ambayo awali iliuzwa Sh10,000 hadi Sh8000, sasa ni kati ya Sh2,000 na Sh3,000, huku kilo iliyouzwa Sh4,000 hadi Sh3,500 ikiuzwa kati ya Sh1,000 na Sh800.

Mwenyekiti wa Soko la Temeke Stereo, Rashid Milao anasema gunia la vitunguu la kilo 100 linauzwa kati ya Sh120,000 na Sh100,000.

Sanduku la nyanya linauzwa kati ya Sh25,000 na Sh20,000.

Milao anasema mkungu wa ndizi ni Sh25,000 hadi Sh20,000, akieleza bei ni rahisi kutokana na maeneo mengi kulima zao hilo.

“Hivi sasa ile kauli kwamba ni msimu wa baridi ndizi hazipatikani haipo, wakulima mikoa mbalimbali wanalima. Wakiona huku kuna baridi wanahamia pasipo na baridi ndiyo maana zinapatika wakati wote,” anasema.

Soko hilo maarufu kwa matunda, kwa sasa embe zinauzwa kati ya Sh700 na Sh800, chungwa kuanzia Sh70 hadi Sh100, huku nanasi kati ya Sh2,500 na Sh3,000.

“Haya ni kwa sababu siyo msimu wake. Matunda ambayo bei yake ni nzuri kwa sasa ni matikitimaji. Hii ni kutokana na mabonde mengi maji yameshatoka, kipindi cha mvua tikiti linalouzwa sasa Sh3,000 lilifika hadi Sh10,000,” anasema.

Juma Dukwe, Mwenyekiti Soko la Nafaka Tandale, anasema bidhaa zimeshuka bei, hali inayotarajiwa kuendelea hadi Septemba.

Anasema mchele uliokuwa ukiuzwa kilo Sh2,000 hadi Sh3,000 sasa ni kati ya Sh1,400 na Sh1,200.

Kuhusu maharage, anasema yaliyouzwa Sh3,500 hadi Sh3,000 sasa ni kati ya Sh2,500 na Sh2,000.

Kwa upande wa mahindi, anasema yameshuka kutoka Sh750 kwa kilo hadi kati ya Sh680 na Sh600.

Jimmy Leonard, mkazi wa Gongo la Mboto, anasema hali iliyo sokoni wanaiona hata mtaani, ambako unga wa sembe walionunua Sh1,500 kwa kilo hivi sasa ni Sh1,000.

Akizungumzia mchele, Maimuna Suleiman, mkazi wa Mbagala, anasema wanapata mpaka wa Sh1,500 kwa kilo, ambao awali uliuzwa kati ya Sh1,800 na  Sh2,000.

Mchuuzi katika duka la rejareja eneo la Chanika, Amri Said, amesema mchele aliokuwa akiuza Sh1,700 kwa kilo sasa anauza Sh1,200.

Kuhusu maharage anasema aliyouza kati ya Sh3,400 na Sh3,500 sasa ni Sh2,600.

Said anasema bidhaa ambayo bado bei ipo juu ni mafuta ya kula, ambayo yaliyokuwa yakiuzwa Sh4,000 kwa lita sasa yamepanda tangu mwaka mpya wa fedha Julai, 2024 na kufikia Sh4,600, huku ya alizeti yakiuzwa Sh8,000 kwa lita bei ya awali. Serikali imeongeza ushuru kwa mafuta yan ayoagizwa kutoka nje.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude anasema bei imeshuka kwa sababu ni msimu wa mavuno.

Hata hivyo, anasema watu watarajie bei hiyo haitakaa muda mrefu sokoni, kwa kuwa ndipo wafanyabiashara wakubwa hununua kwa wingi na kuhifadhi kwenye maghala, ili kuja kuuza bei kubwa baadaye.

Wafanyabiashara wakieleza uchumi wa wananchi si mzuri, Mkude anasema wakulima haohao wanaovuna ndio wanunuzi wa bidhaa, lakini kwa kuwa msimu wa kilimo walikuwa tayari na mikopo ya pembejeo na mbolea wanajikuta hela waliyolipwa baada ya kuuza mazao wanalipa madeni.

Anasema wananchi wa kawaida wengi hawana ajira, hivyo hata kula yao kwa siku ni shida, lakini ndio haohao wanakabiliana na mikopo ya kausha damu mtaani, hivyo ni wazi sokoni licha ya kuwapo bidhaa nyingi hawawezi kupata wateja vile walivyotarajia.

Anashauri wataalamu wa kutafuta namna ya kupata masoko nje ya nchi badala ya kutegemea soko la ndani pekee ambalo mavuno yakiwa mengi vyakula huharibika.

Mkude amewataka wakulima kutafuta mikopo nafuu, akieleza kuna wanaolipa gunia 10 kwa kukopa Sh50,000, akisema mkopo wa aina hiyo hauna tofauti na kaushadamu na kamwe hauwezi kumuinua mkulima alipo.

Mchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai, amesema anachokiona kwa sasa, vyuo vingi vilivyopo Dar es Salaam vimefungwa hivyo hakuna manunuzi yanayofanyika sokoni, hivyo wateja kupungua.

“Mfano mzuri ni wa viazi mbatata, walaji wakubwa wa chipsi ni wanafunzi wa vyuo na sasa hawapo, ni wazi wafanyabiashara wa viazi sokoni lazima waone mabadiliko,” anasema.

Anasema biashara pia imekuwa na watu wa kati wengi kiasi kwamba wanagongana sokoni, huku mkulima hawezi kuona faida ya kilimo.

Anaeleza watu hao huanzia shambani, kwenye usafirishaji mpaka kumfikia mlaji.

Dk Swai anashauri kugeukia biashara ya mazao yaliyosindikwa kuliko kuuza yaliyo ghafi.

“Kama ni ndizi au viazi viwekwe kwenye vifungashio mtu avutike kwenye maduka makubwa, akienda nyumbani yeye ni kupika tu, biashara ambayo wanaifanya wenzetu nchi zilizoendelea tena ni wakulima wenyewe,” anasema.

Anasema lazima wafanyabiashara wabadilike kwa kuwa kizazi cha sasa ndiyo maisha wanayotaka. “Ndiyo maana unaona kuna nyanya za pakiti, nazi vivyo hivyo,” anasema akieleza hilo likifanyika kwenye mazao mengine itaongeza thamani yake.

Related Posts