Familia zapaza sauti wanne wakidaiwa kutekwa, polisi wahusishwa

Dar es Salaam. Matukio ya watu kutoweka katika mazingira yenye kutatanisha huku askari polisi wakihusishwa kuwashikilia yanaendelea kushika kasi nchini.

Taarifa mpya zilizolifikia Mwananchi zinadai kuwa vijana wanne wilayani Temeke, Dar es Salaam na mkazi mmoja mkoani Geita wametoweka na jitihada za kuwatafuta hazijazaa matunda kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Taarifa zinasema vijana Ramadhan Sultan (20), Charles Kelvin (18), Abdulrazack Salim (18), na mwenzao ambaye taarifa zake hazikupatikana, wametoweka tangu Juni 20, 2024.

Wazazi wa vijana watatu waliofika ofisi za Mwananchi zilizoko Tabata Relini, Dar es Salaam, wamesema walichukuliwa na kuingizwa kwenye gari, wakiwa kwenye sherehe kuadhimisha siku ya kuzaliwa rafiki yao iliyofanyika Tandika Maguruwe, Mtaa wa Zone Saba wilayani Temeke.

Inaelezwa saa 2:00 usiku magari mawili yalifika eneo hilo, moja linadaiwa la Jeshi la Polisi na lingine Toyota Noah.

“Ghafla watu watatu walishuka kwenye gari dogo wakiwa kiraia na kuwakamata vijana wetu watatu na huyo mwingine,” anasema Faa Khamis, aliyepotelewa na mwanaye Abdulrazack.

Faa mkazi wa Mtaa wa Yombo, Temeke anasema taarifa za kijana huyo kuchukuliwa alizipata siku ya tukio saa 2:00 usiku alipopigiwa simu na binti aliyekuwapo kwenye sherehe hiyo.

Faa anasema alipoenda eneo hilo alikuta ngoma ikiendelea na kulikuwa na gari la polisi, kisha mwenyekiti wa serikali ya mtaa alifika eneo hilo.

Anadai gari la Polisi lilipoondoka alilifuatilia hadi Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako alielezwa kijana wake hakuwepo, hivyo alienda Kituo cha Polisi Makangarawe nako pia hakumpata.

Faa anadai simu yake muda mwingi iliita pasipo kupokewa.

“Kijana wangu hakuwa na kazi, ingawa kuna wakati alinisaidia shughuli zangu za kibiashara, hasa ninaposafiri kwenda nje ya nchi,” amesema.

Rehema Mcheni, mkazi wa Mbagala Charambe, Mtaa wa Mihanzini anadai taarifa za kutoweka Kelvin alizipata usiku wa Juni 21, kutoka kwa vijana aliokuwa nao kwenye sherehe.

“Asubuhi tulianza kufuatilia vituo vya polisi kila kituo tulikuwa tunajibiwa hayupo, tumezunguka vituo vingi vya polisi Dar es Salaam hatujamuona hadi mochwari zote tumepita hakuna mafanikio,” amesema.

Amesema walifungua taarifa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Anasema kijana huyo alikuwa akiuza mifuko kwenye Soko la Stereo, Temeke.

Mkazi wa Temeke Mikoroshini, Fatuma Abubakari anasema taarifa za kutoweka kijana wake, Sultan alizipata Juni 21, kutoka kwa rafiki zake wakieleza alikamatwa na Polisi.

Anasema wakati anamtafuta kwenye vituo vya polisi alikutana na Faa na Rehema nao wakiwatafuta watoto wao waliopotea siku hiyo ya sherehe.

“Kijana wangu alikuwa anafanya kazi ya bodaboda, lakini mwaka mmoja uliopita alikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kupewa simu kwenda kuuza, kumbe ilikuwa ya wizi. Tangu hapo hajawahi kukutwa na kosa lolote,” anasema.

Kauli ya mwenyekiti wa mtaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Zone Saba, Mohamed Masudi amesema siku ya tukio mtaani hapo kulikuwa na sherehe na kwamba akiwa kiongozi alienda kukagua akakutana na Polisi Kata waliokuwa wakizunguka na gari kuimarisha ulinzi.

“Sasa kusema niliwaona vijana wao au nilikuwepo wakati wanakamatwa siyo kweli. Isipokuwa nilipigiwa simu na Polisi Kata kwenda kuwaangalia watuhumiwa waliokamatwa, kwenye gari niliwaona walikuwa wengi,” amesema.

Masudi amesema hata siku ya pili wazazi hao walipofika ofisini kwake kutoa malalamiko, aliwaelekeza waende kituo cha polisi wakawaangalie akiamini huenda wakawa ni miongoni mwa watuhumiwa aliowaona wamekamatwa na kuwekwa kwenye gari la polisi.

Anasema kabla ya kuwaruhusu kwenda kituo cha polisi aliomba picha zao ili ajiridhishe pengine anaweza kuwafahamu lakini sura zao zote zilikuwa ngeni, akabaini si vijana wa mtaa huo isipokuwa walikuwa wametembelea hapo.

“Hawa vijana wanasema walikamatwa na gari aina ya Noah rangi ya maziwa, sasa siwezi kujua maana siku hizi mambo mengi. Na hapa mtaani kwangu kuna viashiria vya utekaji, kuna kijana mwingine kanusurika kutekwa usiku wa kuamkia leo (Julai 18),” amesema.

Amesema leo asubuhi amepokea simu kutoka Ofisi ya Upelelezi ikimtaka kesho (Julai 19) kwenda Ofisi za Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akieleza hajui sababu hasa ya wito huo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi hilo halihusiki na utekaji lakini taarifa za wazazi hao zimechukuliwa na zinafanyiwa uchunguzi ili wajulikane waliko.

“Jeshi lao liko imara litaendelea kufuatilia kuhakikisha haki zao, ikiwemo haki za wao kuonekana zinakwenda sawasawa,” amesema.

Hata hivyo, Muliro amesema watu wanapaswa kujiuliza maswali kwa nini kila mtu anayepotea wanadhani amechukuliwa na Jeshi la Polisi na wanapaswa kujiuza alikuwa hatari kiasi gani kwa taasisi hiyo hadi achukuliwe na Jeshi.

Daniel Sayi (48), mfanyabiashara wa ng’ombe wilayani Geita anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake katika Kitongoji cha Kiomboi, Kata ya Nyarugusu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana anadaiwa kuchukuliwa Mei 13, 2024 saa 12:00 jioni baada ya watu wanne waliokuwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser jeupe kufika nyumbani kwake, ambako walimfunga pingu na kuondoka naye pasipo kusema chochote.

Familia yake inaeleza imemtafuta kwenye vituo kadhaa vya polisi vikiwamo vya Nyarugusu, Kasamwa, Katoro na Geita hajapatika na hawajui wanaomshikilia. Tukio hilo lipewa taarifa ya polisi namba NGS/RB/230/2024 iliyotolewa na kituo cha Nyarugusu.

Michael, mtoto wa Daniel amesema Mei 13, 2024 akiwa nje ya nyumba yao lilipita gari hilo wakashuka wanaume wanne, kisha likaenda mbele na kugeuzwa.

Anasema watu hao walimuhoji alipo baba yake, akawaelekeza akidhani ni marafiki zake.

“Walinikuta nje barazani, baba alikuwa nyumba kubwa anaangalia mpira. Aliposikia watu wanamuulizia alitoka, walipomuona walimfuata wakamfunga pingu bila kusema chochote, wakamuamuru apande gari ambalo kwa wakati huo lilikuwa limeshaegeshwa getini,” amesema.

Elias Sayi, baba wa Daniel mkazi wa Simiyu, amesema baada ya kupata taarifa hizo alijua amekamatwa na polisi, hivyo aliagiza ndugu zake kwenda polisi kujua kosa lake.

“Mwanangu anajishughulisha na kilimo na biashara ya kununua ng’ombe, wakikua baada ya mwaka anawauza. Sijawahi kupokea malalamiko juu yake,” amesema.

Baba huyo amedai Daniel ni mwanaye pekee wa kiume na sasa analazimika kuwatunza watoto wake 23 ambao bado ni wadogo.

“Hapa tuko kwenye kifungo hatujui hatima, maana angekuwa ameugua na kufa tungezika na kuona kaburi lake lakini sasa nyumba iko kama ina msiba mwili haupo na hatuwezi kufanya chochote. Tunaiomba Serikali itusaidie,” amesema.

Ibrahim Masanja, baba mdogo wa Daniel amesema, “Tumetoa taarifa kila mahali tunachoambiwa ni kusubiri, tumesubiri miezi miwili sasa, lakini hatujapewa mrejesho, polisi wanasema hawajui aliko sasa tunajiuliza nani walimchukua. Tumepewa mpelelezi lakini hata nyumbani hajafika.”

Amesema Daniel mwenye watoto 23 na wake watatu, familia yake imeathirika kisaikolojia.

Salome Nyasika, mke mkubwa wa Daniel amesema maisha yamekuwa magumu kwa kuwa mume ndiye aliyekuwa akiendesha familia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema anafuatilia taarifa hiyo kujua undani wake.

“Nataka nifuatilie nijue waliripoti kituo gani na lini. Wakati mwingine kumekuwa na changamoto, mtu anaweza kuripoti akipotea, lakini akipatikana harudi tena, kumbe alitoka tu na mambo yake, wao wanaona amepotea. Ndiyo maana nasema ngoja nifuatilie,” amesema.

Kufuatia madai hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema kutokana na matukio hayo mamlaka zinatakiwa kufanya uchunguzi wa kina kwa jumla, siyo kwa kuangalia tukio moja.

“Tunatakiwa kuangalia matukio yaliyojitokeza miezi sita iliyopita na kujua kwa nini yanatokea kama ilivyofanyika kwa mauaji ya watu wenye ualbino, tumejua ni ramli chonganishi kwa hiyo tunashughulika na waganga wa jadi,” amesema.

Amesema kuna haja ya kuchukuliwa matukio yote kwa kuangalia moja hadi lingine kujua sababu za kupotea kwao, ilikuwa katika mazingira yapi, na kuwabaini ambao hawajapatikana hadi sasa.

Baadhi ya wadau wa haki jinai wanasema ukamataji wa washukiwa wa uhalifu unaofanywa na polisi bila kuzingatia sheria, unasababisha raia wema washindwe kufahamu kama ndugu yao amekamatwa na polisi kweli au ametekwa nyara na watu wasiojulikana na magenge ya wahalifu yanaweza kutumia mwanya huo  kutekeleza uhalifu huo.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) inataka ofisa wa polisi anayekamata ni lazima amshike bega mtuhumiwa na kujitambulisha kwake na cheo chake na kumjulisha yuko chini ya ulinzi kwa kosa ambalo atamweleza.

Mbali ya hilo, uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu, umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Related Posts