Gamondi awajibu wanaosema amesajili ‘Galacticos’

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amekiri kusikia kelele nyingi kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa soka hasa wale wa Msimbazi wakiponda usajili uliofanywa na klabu hiyo, wakidai wamesajili wazee na kuamua kuwajibu kwa kusema wasubiri msimu uanze ndio watajua hawajui.

Gamondi amesema anashukuru wataufungua msimu kwa kuvaana na Simba na kwa upande wake haangalii matokeo ya msimu uliopita, walipolala kwa penalti 3-1 katika Ngao ya Jamii bali atakomaa na mbinu kuhakikisha Yanga inarudia taji hilo.

Kocha huyo aliyasema hayo muda mchache kabla Yanga haijapaa kwenda Afrika Kusini itakapoweka kambi kwa ajili ya msimu mpya na kesho ikitarajiwa kushuka uwanjani kuvaana na Augsburg ya Ujerumani mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa michuano ya Mpumalanga Cup mechi za michuano hiyo iliyoandaliwa na TS Galaxy kisha kucheza ya tatu na Kaizer Chiefs katika michuano ya Toyota Cup.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu ratiba ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao ni mabingwa watetezi alisema ni mchezo mwingine tofauti na msimu uliopita.

“Wanaweza kusema tumesajili wazee, lakini ukweli ni nina kikosi bora na ninakiamini wakati tunaenda kujiandaa zaidi nje ya nchi kabla ya kuja kucheza mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Simba ni timu nzuri tutacheza nao Ngao ya Jamii, japo sitaangalia matokeo ya mchezo uliopita, siuchukulii mchezo huo kwa ukubwa, ila natamani tupate matokeo na malengo yetu makubwa ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu. Muhimu ni kusubiri kuona itakuwaje.”

Gamondi ameondoka na karibu jeshi lake lote wakiwamo mashine mpya zilizosajiliwa hivi karibuni kama Prince Dube, Duke Abuya, Clatous Chama, Aziz Andambwile, Jean Baleke, Abubakar Khomeiny na Chadrack Boka sambamba na nyota wa msimu uliopita Stephane Aziz KI, Khalid Aucho, Yao Kouassi, Kennedy Musonda, Djigui Diara, Jonas Mkude, Salum Abubakar ‘Sureboy’, huku Pacome Zouzoua akikosekana bila kuwepo kwa taarifa kwa nini kiungo mshambuliaji huyo hayupo kwenye msafara huo.

Kumekuwa na maswali mengi juu ya kushindwa kutambulishwa kwa Jean Baleke licha ya straika huyo wa zamani wa Simba kuonekana mazoezini na kuwa kwenye msafara wa Yanga unaoenda Afrika Kusini na Mwanaspoti likajaribu kuchimba kujua ukweli.

Inaelezwa pamoja na Baleke kupewa mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, pia bado ni mchezaji wa TP Mazembe, hivyo klabu zinazomhitaji lazima zizungumze na wahusika, hata hivyo Yanga imemalizana na klabu hiyo ya DR Congo, lakini tatizo lipo kwa Al Ittihad ya Libya aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo.

Mwanaspoti limejua Baleke, alibakiza mkataba wa miezi sita na Al Ittihad, kwani alisaini mwaka mmoja na ametumikia nusu, hivyo inawia ngumu Yanga kutangaza kwa sababu itaonekana imesajili mchezaji wa klabu nyingine na itaingia kwenye mgogoro na Walibya.

Chanzo cha taarifa hiyo kinasema, “Yanga tumemalizana na TP Mazembe, ishu inakuja timu aliyotokea ndio tunashughulikia hilo, ili tuwe huru na mchezaji wetu. Ndio maana amerudishwa Kennedy Musonda ambaye tulikuwa na lengo la kuachana naye, lakini nisisitize tunaendelea kulishulikia.” 

Related Posts