Hukumu kesi ya Milembe yaahirishwa, sababu yatajwa

Geita. Hukumu ya kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa wanne wanaodaiwa kumuua Milembe Suleman (43), iliyopangwa kutolewa leo imeahirishwa hadi Agosti 23, 2024.

Wakati inaahirishwa si washtakiwa wala mawakili wapande zote waliokuwepo mahakamani saa tatu asubuhi ya leo, Julai 19, 2024, muda uliokuwa umepangwa.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Meritho Ukongoji akizungumza kwa simu na Mwananchi amesema kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 23, 2024 itakapokuja kwa ajili ya hukumu kutokana na Jaji aliyekuwa akiisikiliza kuwa safarini kikazi.

Mwananchi Digital imezungumza pia na Wakili wa mshtakiwa wa pili, Laurent Bugoti ambaye amesema alikuwa anajiandaa kwenda mahakamani, akapigiwa kuelezwa kuwa kesi hiyo haitaendelea leo.

Hata hivyo, amesema hajaelezwa sababu za kesi kutoendelea ingawa amedokeza mawakili wana taarifa za jaji anayeisikiliza kuwa safarini.

Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 iko chini ya Jaji Mfawidhi Kelvin Mhina ambaye tayari amesikiliza ushahidi wa pande zote mbili na leo ilikuwa atoe hukumu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastory na Musa Pastory (33), wote ambao kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Suleman kwa kukusudia.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts