Kikongwe wa miaka 90 afariki dunia kwa shambulio la nyuki

Arusha. Vilio na simanzi vimetanda katika boma la Mitong’ori lililopo katika Kata ya Olturoto wilayani Arumeru baada ya nyuki kumvamia na kusababisha kifo cha Penina Tadayo (90).

Penina amefariki dunia leo Julai 19, 2024 wakati akipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa matibabu baada ya kuvamiwa na nyuki hao alipokwenda shambani kuchimba magimbi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema tukio hilo amelisikia na analifuatilia kujua undani wake.

“Hata mimi nimesikia kama unavyonieleza, sijui undani wake sana maana tuko kwenye maandalizi ya mapokezi ya mwenge,” amesema Masejo.

Mtoto wa marehemu, Obed Alfayo (61) amesema saa 9 alasiri, akiwa nyumbani kwake (jirani na kwa marehemu), alisikia ukunga ukitokea mashambani na alipofika eneo ilikotokea sauti hiyo, akakuta mama yake ameanguka chini ya moja ya miti yenye mizinga, huku akishambuliwa na nyuki.

“Nilimkimbilia mama yangu na kuanza kumburuza kumtoa eneo la tukio, wakati watu wengi wakiwa wamefika lakini hakuna hata mmoja alithubutu kusogea.

Baada ya kumsogeza na nyuki kupungua, ndipo watu wengine wakasogea kunisaidia” amesema Obed ambaye pia amejeruhiwa sehemu za mikononi na usoni.

Amesema wakati wanampeleka hospitalini kwa matibabu mama yake alikuwa amekwishapoteza fahamu, baadaye alifariki dunia wakiwa njiani.

“Nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kuokoa maisha ya mama yangu, hata nilivyoishiwa nguvu nilitoa sauti ya juu kuomba watu wanisaidie, lakini hata hivyo haikuwa bahati tena mimi kuwa na mama duniani,” amesema Obed na kuangua kilio upya.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngiresi kilichopo kata ya Olturoto, Lothy Sareiyo amesema majira ya jioni alipigiwa simu na wasamaria wema kuwa Bibi wa Boma la Mitong’ori amevamiwa na nyuki, aliwahi eneo la tukio la kuungana na wananchi kutoa msaada.

“Nilikuta watu wamezingira eneo la tukio wakiwa wamewasha moto ili kufukuza nyuki, huku wengine wakisaidiana kumpa huduma ya kwanza bibi huyo,” amesema mwenyekiti huyo.

Jirani wa boma la marehemu, Pamela Daudi amesema walipofika eneo la tukio walimkuta Obed (mtoto wa marehemu) akiwa anamburuza mama yake kumwokoa na nyuki.

“Mama yake (Obed) alikuwa amezingirwa na nyuki kila upande wa mwili wake, ili kumtoa eneo lenye mizinga ndio tukaongeza ukunga watu wengi wakaja kumsaidia.

“Bibi huyu huwa ana kawaida ya kuingia shambani kila jioni kuchimba magimbi au kuokota kuni, na pia aliwahi kuvamiwa na nyuki siku za nyuma lakini hakudhurika sana,” amesema Pamela.

Related Posts