Dar es Salaam. Msanii wa zamani wa Kaole na mwigizaji wa filamu nchini, Dorah Mwakatete maarufu kama Kadadaa, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo, Dar es Salaam na kusomewa shtaka moja la wizi wa Sh4.6 milioni.
Kadadaa ambaye aliwahi kuwika katika uigizaji miaka ya 2000 akiwa na kundi la Kaole, amefikishwa mahakamani hapo leo, Julai 19, 2024 na kusomewa shtaka hilo na karani Aurelia Bahati, mbele ya Hakimu Gladnes Njau.
Bahati amedai kuwa Juni 26, 2023 saa 10:00 alasiri katika jengo la PSSSF Tower, Mtaa wa Samora lililopo wilaya ya Ilala.
Alidai siku hiyo ya tukio, mshtakiwa aliiba Sh4,658,000 mali ya Feisal Sonzera huku akijua kitendo hicho ni kosa kisheria.
Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shtaka hilo amekana kutenda kosa hilo na kuomba apatiwe dhamana.
Hakimu Njau amesema shtaka linalomkabili Kadadaa linadhaminika na hivyo amempa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vinavyotambuliwa kisheria, watakao saini bondi ya Sh3 milioni kila moja.
Mshtakiwa ametimiza masharti ya dhamana na kuachiwa. Hakimu Njau ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 29, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji.
Dorah alijiunga na kikundi cha uigizaji cha Kaole mwaka 2002 na kushiriki katika baadhi ya tamthilia na filamu akiwa na wasanii wakubwa kama Marehemu Steven Kanumba, Vincent Kigosi na wengineo.
Baadhi ya tamthilia alizoshiriki ni Radio, Jahazi, Dira, Zizimo, Taswira, Ghalika, Tufani, Baragumu na filamu alizocheza ni My wife, Sikitiko langu, Dar to Lagoz, Penina, Dangerous desire, Family tears, Full moon, Woman of principle, White Maria, My Pastor na nyingine.