TETESI ZA USAJILI BONGO:Kramo kurejea ASEC,Mangolo kutolewa kwa mkopo Botswana

MABOSI wa Singida Black Stars wamepanga kumtoa kwa mkopo beki wa kushoto, Benson Bolasie Mangolo kwenda Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Raia huyo wa Botswana alisajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea Jwaneng Galaxy, lakini amekuwa akivutana na viongozi akitaka atemwe moja kwa moja licha ya kuwa na mkataba wa mwaka mmoja, huku klabu ikitaka kumtoa kwa mkopo hadi mkataba huo utakapomalizika.

Singida inataka kumtoa kwa mkopo beki huyo baada ya kumsajili hivi karibuni, Mghana Ibrahim Imoro aliyewahi kukipiga Al Hilal ya Sudan.

BUNDA Queens inaripotiwa imeanza mazungumzo na kipa wa Baobab Queens iliyoshuka daraja, Jeanne Pauline. Kipa huyo Mnyarwanda licha ya kubakiza mkataba wa mwaka mmoja na Baobab, lakini klabu hiyo imemuachia huru kutafuta timu nyingine.

SIMBA Queens imekamilisha usajili wa beki wa kati wa zamani wa Yanga, Emiliana Mdimu aliokuwa anakipiga Ceasiaa Queens ya Iringa.

Awali Fountain Gate Princess, Heroes Queens zilikuwa zikiwania saini ya beki huyo mwenye uwezo pia wa kucheza pembeni lakini Simba ikafanikisha.

INADAIWA Yanga Princess imetibua mipango ya Ceasiaa Queens kwa beki wa kushoto, Silivia Mwacha aliyemaliza mkataba na Simba. Kuna uwezekano mkubwa wa beki huyo kujiunga na Yanga msimu ujao kutokana na ofa aliopewa ingawa bado mazungumzo yanaendelea.

PUNDE baada ya kumtambulisha kiungo mshambuliaji wa Ceasiaa Queens, Janet Matulanga inaelezwa JKT Queens imerudi kumuulizia kupata saini ya beki, Kija John. Matamanio ya JKT ni kuhakikisha inampata beki huyo ambaye atakwenda kusaidiana na Christer Bahera eneo la ulinzi.

BAADA ya kumalizana na Simba, winga Aubin Kramo inadaiwa yupo hatua za mwisho kurejea Asec Mimosas ya Ivory Coast aliyokuwa akiichezea kabla ya kusajiliwa Msimbazi. Inadaiwa Asec imeanzisha mazungumzo na Krabo na licha ya awali kudaiwa huenda angeenda klabu za Afrika Kaskazini, dili hilo lipo pazuri.

GEORGE Mpole aliyekuwa akifukuziwa na Yanga, huenda akaibukia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku pia Richards Bay pia ya Sauzi na Singida Black Stars zikitajwa. Mpole alikuwa akikipiga FC Lupopo na Yanga ilikuwa katika mazungumzo naye kabla ya kushindwa na sasa inaelezwa huenda akaibukia Sauzi.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Mtibwa Sugar, aliyekuwa kikipiga Ihefu (sasa Singida BS), Masoud Kibaya  anatajwa kuwa mbioni kutua KenGold. Inadaiwa mabosi wa KenGold ambao wanafanya usajili wao kimyakimya wamewasiliana na Kibaya ili ajiunge nayo kwa msimu ujao. Kagera Sugar na Pamba Jiji nazo zinamnyemelea.

Related Posts