AKAMATWA AKIDAIWA KUJARIBU KUTEKA WATOTO WAWILI – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Kijana ambaye jina lake halikupatikana amekamatwa na wananchi na kupelekwa kituo kidogo cha polisi Tabata Kisiwani akituhumiwa kujaribu kuiba watoto waliokuwa wakienda shuleni.

 

Tukio hilo limetokea Julai 23, 2024 baada ya wananchi wa eneo la Tabata Kisiwani kudai kijana huyo ni mgeni machoni mwao na kwamba alionekana asubuhi akiranda mtaani hivyo kutiliwa shaka.

 

Kwa mujibu wa taarifa mtaani hapo, baadaye alionekana akiwa na mtoto mdogo wa darasa la nne akiwa amembebea begi.

 

Inadaiwa na wananchi alipoulizwa iwapo anamfahamu mtoto huyo alijibu, “kwani vipi.” Kwa majibu hayo, inadaiwa baba mzazi wa mtoto huyo alimchukua mwanaye na kumpeleka shule.

 

Inadaiwa baada ya muda kidogo, alionekana akimbeba mtoto mwingine aitwaye Ikram Said mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minne na kutaka kuondoka naye.

 

Kwa maelezo ya wananchi, kaka wa mtoto huyo alipiga kelele, hivyo alimuachia na kuanza kukimbia.

 

Inadaiwa mama mzazi wa Ikram akishirikiana na majirani na sungusungu (ulinzi shirikishi) walimkamata na kumpeleka kituo cha kidogo cha polisi Tabata Kisiwani.

Related Posts