Israel imeyalaani makubaliano ya Wapalestina ya kuleta umoja na maridhiano, yaliyofikiwa leo huko Beijing.
Israel imemkosoa vikali rais Mahmoud Abbas ambaye chama chake cha Fatah kimeridhia kufanya kazi kwa pamoja na Hamas na makundi mengine, kuitawala mamlaka ya Wapalestina.
Maridhiano ya Wapalestina yamekuja katika kiwingu cha mashambulio ya Israel yanayoendelea kufanywa Ukanda wa Gaza.
Muda mfupi baada ya Makundi 14 ya Wapalestina kusaini makubaliano ya kuwa na serikali ya maridhiano ya kitaifa leo Jumanne huko Beijing, Israel imeshatowa tamko,ikionesha kughadhabishwa na hatua hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Israel Katz amesema utawala unaolihusisha kundi la Hamas utasambaratishwa huku akimshutumu rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas ambaye chama chake cha Fatah pia kimesaini makubaliano hayo.
Israel yawapa Onyo Wapalestina kuhusu ushirikiano na Hamas
Israel imesema serikali yoyote itakayoundwa baada ya vita katika Ukanda wa Gaza na kulihusisha kundi la wanamgambo la Hamas itakuwa inakwenda kinyume na Marekani na Israel.
China ambayo imesimamia mchakato huo wa maridhiano ya Wapalestina imeyaita makubaliano hayo kuwa muhimu yatakayofungua njia ya kupatikana amani na utulivu mashariki ya kati, kama alivyofafanuwa waziri wake wa mambo ya nje Wang Yi.
“China iko tayari kuimarisha mawasiliano na kuzileta pande zote pamoja katika utekelezaji wa azimio la Beijing lililofikiwa leo na kuchukuwa dhima muhimu katika kudumisha amani na uthabiti katika Mashariki ya kati.”
Hatua iliyofikiwa Beijing imekuja wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa Washington,Marekani ambako anatarajiwa kulihutubia bunge na ameapa kuendelea na vita vya Gaza hadi atakapoliangamiza kundi la Hamas.
Kundi hilo na chama cha Fatah kwa muda mrefu walikuwa mahasimu waliowahi kupigana kwa muda mfupi katika vita vilivyosaabisha umwagaji mkubwa wa damu mnamo mwaka 2007,kipindi ambacho Hamas walifanikiwa kutwaa udhibiti wa Gaza.Soma pia: Wapalestina wakubaliana kuunda serikali ya maridhiano itakayohusisha Hamas na Fatah
Kundi la Hamas linasema kupitia maridhiano ya Beijing linaimani ukurasa mpya umefunguliwa kwa Wapalestina.Moussa Marzouk ni kiongozi wa ngazi za juu wa kisiasa wa kundi hilo.
“Leo tunaposaini makubaliano ya Umoja wa Kitaifa tunachosema ni kwamba,njia ya kuikamilisha safari hii ni Umoja wetu wa kitaifa na kwahivyo tunajitolea kwa mshikamano wa kitaifa na kuuombea, usiingiliwe na chochote cha kuhujumu Umoja huu .”
Azimio la Beijing linafafanuwa kwamba serikali ya muda itakayoundwa chini ya makubaliano ya makundi yote ya Palestina yaliyosaini azimio hilo itakuwa na mamlaka ya uongozi wa Palestina kuanzia Ukanda wa Gaza hadi Ukingo wa Magharibi ikiwemo ardhi ya Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Israel,Israel Katz amepinga hatua ya kupelekwa utawala wa Wapalestina Gaza akisema rais Mahmoud Abbas hatoruhusiwa kuijongelea Gaza.
Katz amemshambulia rais Abbas akisema anawakumbatia Hamas ambao amewataja kama wauwaji na wabakaji.Soma pia: Vikosi vya Israel vyaendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza
Katika uwanja wa vita huko Gaza,Israel imeendelea leo kuporomosha mabomu ikiwemo katika mji wa kusini wa Khan Yunis ambako jana iliwataka Wapalestina waondoke.
Jeshi la Israel limesema madege yake ya kivita na vifaru vimeshambulia maeneo 50 ya magaidi na kuwauwa wanamgambo kadhaa katika operesheni hiyo ya Khan Yunis.