Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Tanzania (DCI), Ramadhan Kingai ni miongoni mwa mashahidi 40 wa Serikali wanaotarajia kutoa ushahidi katika kesi ya mauaji inayomkabili mama na mtoto wake wa kiume.
Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kuwa mashahidi hao na vielelezo 11 vinatarajia kutolewa katika kesi ya mauaji inayomkabili, Alphonce Magombola (36) na mama yake mzazi, Sophia Mwenda (64), wanaodaiwa kumuua mwanafamilia mwenzao, Beatrice Magombola.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika na kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Wakili wa Serikali, Asiath Mzamiru, ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumanne Julai 23, 2024 wakati akiwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Wakili Mzamiru amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo kuwa, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji.
Amedai, Mwenda ambaye ni mkazi wa Mbagala anadaiwa kushirikiana na mtoto wake huyo wa kiume kumuua Beatrice Magombola ambaye ni binti yake wa kumzaa mwenyewe.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, Desemba Mosi, 2020 katika eneo la Kijichi wilayani Temeke.
Maelezo ya mashahidi na vielelezo:
Akiwasomea maelezo hayo, Mzamiru amedai Machi 16, 2020 saa nne asubuhi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai, alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kupotea kwa Beatrice Magombola.
Msiri huyo, alidai kulikuwa na taarifa za utata kuhusu kupotea kwake kwa kuwa mama mzazi wa Beatrice aitwaye Sophia (mshtakiwa wa pili), alidai mtoto wake amekwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, lakini wakati mwingine alipohojiwa alidai Beatrice amekwenda nchini Canada kutibiwa.
“Msiri huyo alidai mama huyo alipoulizwa alipo mtoto wake alikuwa anatoa majibu tata yakiwamo ya kudai kuwa mtoto wake huyo yupo Afrika Kusini na wakati mwingine alidai kuwa yupo Cadana kwa ajili ya matibabu” amedai Wakili Mzamiru.
Mzamiru aliendelea kudai kuwa, hata mama huyo hakuweka wazi ugonjwa unaomsumbua Beatrice na taarifa za ugonjwa hazikuwa zikifahamika kwa ndugu wala baba yake mzazi isipokuwa kaka yake mkubwa Alphonce, ambaye ni mshtakiwa namba moja.
“Msiri huyo aliendelea kudai, Beatrice alikuwa na gari aina ya Toyota Vanguard lililokuwa likitumiwa na Alphonce na pia nyumba yake iliuzwa na Sophia na kuna wakati washtakiwa hao walipohojiwa kupotea kwa Beatrice wanakuwa wakali,” amedia wakili.
Mahakama hiyo iliendelea kueleza kutokana na msiri huyo kutoa taarifa hizo, Kamanda Kingai alielekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi na upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kukamatwa kwa washtakiwa hao.
Hata hiyo, kwa mujibu wa maelezo ya onyo ya washtakiwa wote kwa pamoja, walikiri kumuua Beatrice kwa kumchoma kwa kisu katika titi la kushoto.
Inadaiwa wakati wa kutekeleza mauaji hayo, Alphonce alimfunga miguu na kumshika mikono huku Sophia alimchoma choma kwa kisu hadi alipofariki dunia.
Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa, baada ya kumuua washtakiwa waliuzungusha mwili wa Beatrice kwa shuka na mkeka wa kichina na kisha kumfunga vizuri na kwenda kuutupa eneo la Zinga, lililopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa sababu ya kumuua Beatrice ni kutokana na kutaka kwenda kutoa ushahidi mahakamani Mbeya katika kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao.
Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo walikana shtaka hilo na kukubali majina na taarifa binafsi.
Hakimu Swallo baada ya kumaliza kusikiliza maelezo hayo aliihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu na washtakiwa hao wataendelea kubaki rumande hadi hapo Mahakama Kuu itakapo panga tarehe kwa ajili ya kusikilizwa.
Siku ya kwanza washtakiwa kufikishwa Kisutu:
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu Julai 15, 2022 na kusomewa kesi ya mauaji namba 3 ya mwaka 2022.
Hata hivyo, kwa muda wote huo, washtakiwa hao walikuwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili kutokuwa na dhamana.