Geay awatoa hofu Watanzania kuhusu Olimpiki

MUDA mfupi baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay huenda asikimbie katika mashindano ya Olimpiki yanayotarajiwa kuanza wiki hii nchini Ufaransa, mwenyewe ameibuka na kuwatoa hofu Watanzania.

Taarifa za awali zilizonukuliwa na Mwanaspoti kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) zilidai kwamba mwanariadha huyo ni majeruhi, lakini atakwenda Paris, Ufaransa inakofanyika michuano hiyo huku kukiwa hakuna uhakika wa asilimia kwamba angeshiriki kutokana na kuwa majeruhi.  

Hata hivyo, Geay amewatoa hofu wadau wa michezo kutokana na majeraha ambayo yanamkabili, akisisitiza kwamba  afya yake inazidi kuimarika, hivyo anaamini atashiriki mashindano hayo.

Nyota huyo ni miongoni mwa wanariadha wanne ambao wataiwakilisha Tanzania katika mbio za marathoni za Olimpiki ambazo zitafanyika Agosti 10 na 11, mwaka huu nchini humo.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu kusumbuliwa na majeraha ya mguu, Geay amesema afya yake inazidi kuimarika na tayari amefanyiwa uchunguzi na daktari wa timu ya taifa na kuambiwa afanye mazoezi kwa kiwango ambacho siyo cha juu sana.

Lakini pia, ameambiwa kwamba mazoezi hayo yanapaswa kuwa laini ambayo yatamfanya asiendelee kuwa na majeraha makubwa zaidi.

“Kulingana na maelekezo yake na mimi nafanya hivyo na naamini kwamba inapofika kwenye haya mashindano nitakuwa sawa”, amesema Geay.

Ameongeza kuwa anapaswa kufanya maandalizi kwa namna ambayo inatakiwa ili kwenda kufanya vizuri Olimpiki, huku akiamini kwamba ataonyesha juhudi endapo atafanikiwa kukimbia.

Mapema leo daktari wa timu ya Tanzania kwenye michezo hiyo, Eliasa Mkongo amekaririwa akisema nyota huyo atasafiri na timu kwenda Paris, lakini ana maumivu ya mguu wa kulia kwenye kifundo na kwamba anaendelea kuangaliwa kwa ukaribu kama atamudu kukimbia au la.

“Kwa jinsi hali yake ilivyo na siku zilizosalia kabla ya mbio ya marathoni kuna uwezekano mkubwa afya yake ikaimarika na kukimbia,” amesema daktari huyo.

Katika michezo ya Olimpiki ambayo itaanza Julai 26 Tanzania itawakilishwa na wanamichezo saba wa michezo mitatu wakiwamo wanariadha wanne, judo mmoja na kuogelea wawili, huku wanariadha wakiwa ni Alphonce Simbu, Geay, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri.

Wengine ni Collins Saliboko, Sophia Latiff wa kuogelea pamoja na Mlugu Andrew Thomas wa Judo.

Related Posts