Geay hatihati Olimpiki, daktari afunguka

Kuna hatihati kwa nyota wa Tanzania wa mbio za marathoni, Gabriel Geay kushindwa kuchuana kwenye Olimpiki msimu huu kutokana na kuwa majeruhi.

Hata hivyo, daktari wa timu ya Tanzania kwenye michezo hiyo, Eliasa Mkongo amesema nyota huyo atasafiri na timu kwenda Paris, Ufaransa inakofanyika michezo hiyo itakayofunguliwa Julai 26.

Amesema, Geay ambaye ana maumivu ya mguu wa kulia kwenye kifundo anaendelea kuangaliwa kwa ukaribu kama atamudu kukimbia akiwa Paris au la.

“Kwa jinsi hali yake ilivyo na siku zilizosalia kabla ya mbio ya marathoni kuna uwezekano mkubwa afya yake ikaimarika na kukimbia,” amesema daktari huyo.

Geay ni miongoni mwa wanariadha wanne waliofuzu kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki msimu huu huku wengine wakiwa ni Alphonce Simbu, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao watakimbia Agosti 10 na 11.

Wanariadha hao wataondoka nchini Agosti 7 kwenda Paris wakati timu nyingine ya Tanzania ya judo na kuogelea pamoja na watu wengine wakiondoka leo Julai 23, 2024.

Akizungumza kabla ya kuondoka, Dk Mkongo amesema kwa majeraha aliyonayo Geay anaweza kuendelea na matibabu na kuimarika kwa siku zilizosalia akakimbia kwenye Olimpiki .

“Amekuwa mwenye majeraha hayo kwa wiki mbili ambayo kwa wanariadha wa mbio ndefu hayo ni maumivu ya kawaida. Geay ana maumivu lakini si kwa kiwango cha juu. Amekuwa anapata maumivu akishamaliza kufanya mazoezi, lile eneo la kifundo linavimba,” amesema daktari huyo.

“Siku timu inaagwa (Ijumaa iliyopita) Geay hakuwepo alikuwa anafanya baadhi ya vipimo, ikiwamo cha MRI tulivyoshauriana mchezaji mwenyewe alikuwa tayari kuwakilisha nchi yake kwenye Olimpiki.”

Amesema amemshauri apumzike kidogo na wameona ni vyema asafiri na timu kwa kuwa nchini Ufaransa kuna madaktari wote, hivyo itampa nafasi ya kufanyiwa vipimo vyote na kwa muda uliobaki kabla ya mbio ya marathoni wanatarajia atapata nafasi ya kushiriki.

Wakizungumzia kusafiri na timu kwa Geay, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema wameshauriana mwanariadha huyo asafiri akiendelea kuimarika na huenda itakapofika mashindano yake atakuwa sawa.

“Taarifa yake ya kuumwa tumeipata siku timu inaagwa. Tulijua anaendelea na mazoezi na pesa ya mwisho ya maandalizi kwa wale wanaofadhiliwa na Olympic Solidarity akiwamo Geay walipewa wiki mbili zilizopita,” amesema.

Bayi amesema kwa wanariadha wa mbio ndefu si jambo la kushangaza kupata maumivu ya miguu, wanapopumzika wengi wanarudi kwenye hali ya kawaida.

“TOC tulipoambiwa Geay ana majeraha hayo tulimtuma daaktari kwenda Arusha kuchukua vipimo ili tuone tunamsaidiaje ku-recover. Daktari ameshauri aende na timu Paris kule kuna madaktari wa kila na kuna uwezekano hadi kufika siku ya mbio yake atakuwa ameimarika,” amesema.

Rais wa TOC,  Gulam Rashid amesema kwenda kwa Geay Paris ni kuangalia kama ataimarika na kupata madaktari zaidi wa kumtibu akiwa kule.

“Kukimbia au kutokimbia itategemea na afya yake itakavyokuwa. Taratibu zake za safari zilishafanyika na hata asipokwenda hakuna ambacho kitapunguza gharama au kuongeza kama atakwenda.

“Hata kama hatashiriki mbio yake, hiyo itakuwa ni nafasi nzuri kwq yeye kuonana na madaktari kule ili kuangalia zaidi afya yake, tunachojua Geay yupo kwenye safari na hakuna tunachoweza kupoteza hata asipokwenda Paris,” amesema Gulam.

Related Posts