Hatima ya Mwabukusi urais TLS Ijumaa

Dar es Salaam. Hatima ya Wakili Boniface Mwabukusi kugombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) sasa itajulikana Ijumaa hii ya Julai 26, 2024, wakati Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa shauri lake la kupinga kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.

Uamuzi huo unaotarajiwa kutolewa siku hiyo na Jaji Butamo Phillip ndio utakaotoa hatima ya Mwabukusi katika kinyang’anyiro hicho.

Mwabukusi alikuwa mmoja wa wanachama waliomba na kupitishwa na Kamati ya Uchaguzi kugombea nafasi ya urais wa TLS, unaotarajiwa kufanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma lakini aliondolewa katika kinyang’anyiro hicho na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa dhidi yake.

Katibu wa Kamati Uchaguzi wa TLS ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TLS, Nelson Frank alilieleza Mwananchi Wakili Mwabukusi aliondolewa katika kinyang’anyiro hicho baada ya Kamati hiyo kujiridhisha hana sifa kwa mujibu wa Kanuni.

“Mwabukusi anakosa sifa moja katika kanuni ya 13 (c) kwa sababu alishatiwa hatiani kwenye Kamati ya Maadili, akapewa adhabu ya onyo na hiyo hukumu bado haijatenguliwa, hivyo bado ana doa la kimaadili kinyume na kanuni hiyo ya 13.

Hata hivyo, Mwabukusi hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo alifungua shauri la maombi Mahakama Kuu Dar es Salaam, akaomba ridhaa ya kupinga uamuzi huo kwa njia ya shauri la maombi ya mapitio ya mahakama na amri ya zuio la muda la uchaguzi huo.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa Julai 17, 2024 na Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza maombi hayo ilimkatalia ombi la amri ya zuio la muda la uchaguzi huo lakini ikamruhusu kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama, kupinga kuenguliwa kwake ndani siku 14.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Julai 23, 2024, Mwabukusi amesema baada ya kupata ridhaa hiyo tayari alishafungua shauri hilo na kwamba lilishasikilizwa na mahakama imepanga kutoa uamuzi Ijumaa Julai 26, 2024.

“Nimeshafungua na kusikilizwa na Jaji Phillip uamuzi unakuja Ijumaa hii ya tarehe 26, saa tatu asubuhi,” amesema Mwabukusi.

Mmoja wa mawakili wa Mwabukusi, Edward Heche amelieleza Mwananchi shauri hilo lilishafunguliwa tangu siku ya shauri la maombi ya ridhaa liliposikilizwa na kuamuriwa, Julai 17 na kwamba shauri hilo la mapitio lililisikilizwa jana Jumatatu.

Mbali na Heche, Mwabukusi anawakilishwa na jopo la mawakili 29, linaloongozwa na Mpale Mpoki. Mawakili wengine baadhi yao ni Peter Kibatala, Jebra Kambole, Dickson Matata, Aziza Msangi na Happiness Michael.

Katika shauri hilo Mwabukusi na wengineo anaiomba mahakama itoe amri ya kutengua uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TLS, pamoja na mambo mengine akidai kuwa unakiuka misingi ya kanuni ya haki asili kwa kuenguliwa bila kumpa haki ya fursa ya kusikilizwa.

Iwapo mahakama itakubaliana na hoja zake za kupinga kuenguliwa kuwa haikuwa sababu za kumuengua hazikuwa halali, basi mahakama hiyo kupitia uamuzi huo itatoa amri ya kurejeshwa katika kinyang’anyiro hicho kwenda kuchuana na wagombea wengine wa nafasi hiyo.

Wagombea wengine wa nafasi hiyo ya urais wa TLS ni makamu wa rais wa zamani wa TLS, Ibrahim Bendera, Revocatus Kuuli, Emmanuel Muga, Sweetbert Nkuba na Paul Kaunda.

Related Posts