HISIA ZANGU: Kibu Dennis, udhaifu wetu katika mambo ya msingi 

MARA ya mwisho alitokomea katika kambi ya Taifa Stars pale Jakarta, Indonesia miezi miwili iliyopita. Staa mpya katika soka letu. Kibu Dennis. Alitoa sababu kwamba asingeweza kujiunga na kambi ya Stars kwa sababu mwili wake ulikuwa umechoka.

Kwamba alihitaji kwenda Marekani kupumzisha mwili wake. kwanini asiende na pesa anayo? Si ndio ulikuwa wakati ule Simba walipoingiza noti nyingi katika akaunti yake baada ya kuzuka uvumi kwamba huenda Yanga wangemchukua.

Wakati Kibu anadai kwamba mwili wake ulikuwa umechoka na asingeweza kwenda Indonesia, Kevin de Brune, Kylian Mbappe, Cristiano Ronaldo na mastaa kibao wakubwa barani Ulaya walikuwa wanajiandaa kucheza michuano ya Euro. Tena wana idadi kubwa ya mechi za msimu ulioisha kuliko Kibu.

Na sasa Kibu amepotea pia katika kambi ya Simba. Majuzi nikasikia kwamba alikuwa na tatizo na pasipoti yake. kwamba imejaa. Kisingizio cha zamani hiki ambacho kingeweza kutumika wakati Juma Magoma akiwa shule ya msingi na watu wangekuelewa.

Zamani pasipoti zilikuwa na ugumu wake kidogo. Siku hizi ni jambo dogo. Idara ya Uhamiaji inafanya mambo kisasa zaidi. Mchezaji kama Kibu sababu zake zinajulikana wazi wazi hadi katika vyombo vya habari. Maofisa wanaweza kumpokea pale wakiwa na tabasamu kubwa na ndani ya saa 72 anapata hati yake ya kusafiria.

Wachezaji, wasanii, waandishi wa habari na watu maarufu wamekuwa wakipewa ushirikiano mzuri na wa kipendeleo zaidi kupata hati zao za kusafiria. Kwa Kibu hilo ni jambo dogo tu. Mchakato wa visa ya Misri nao ni jambo la saa 24 tu. Kwanini hadi wakati naandika Kibu bado hayupo kambini Misri?

Kama hiyo haitoshi nilisikia minong’ono kwamba huenda Kibu amepata timu barani Ulaya. Vyovyote ilivyo atakuwa amepishana na gari la mshahara. Ingekuwa hajasaini Simba, basi ingekuwa rahisi kuondoka zake kama mchezaji huru. Lakini sasa Simba wana mkataba wake.

Simba ndio ambayo inaweza kuamua kumuuza au vinginevyo. Hana tena nafasi ya kuondoka kama mchezaji huru. Huwa inatokea. Ni kama ilivyowatokea Coastal Union kwa Lameck Lawi. Walipomuuza kwenda Simba tu ndipo ikatokea timu kutoka Ubelgiji. Nadhani ndio maana walirudisha pesa za Simba.

Kuna mambo mawili ambayo inabidi tujifunze katika mpira wetu. Maisha ya mchezaji na klabu. Simba walipaswa kulitolea ufafanuzi suala la Kibu kwa muda mrefu. Kama haufanyi hivyo ni wazi kwamba unawayumbisha mashabiki.

Mashabiki wana haki ya kupewa taarifa kuhusu wachezaji wao. Hata kama taarifa yenyewe ni fupi na inayojaribu kuficha mambo mengi. Kule kwa wenzetu huwa tunaona taarifa mbalimbali zinazohusu kukosekana kwa wachezaji. Iwe kwa majeraha, iwe kwa kadi za uwanjani au matatizo ya kifamilia.

Tumekuwa wepesi katika kuwalilia mashabiki waje uwanjani au wanunue jezi ama walipie mitandao inayotoa taarifa za klabu. Hata hivyo kuna eneo hili ambalo hatuwatendei haki mashabiki na wanachama. Mfano halisi ni suala hili la Kibu.

Mwisho wa siku jambo kama hili huwa linavunja morali ya timu kutoka kwa mashabiki kuelekea katika msimu mpya. Msimu uliopita hali ilikuwa kama hivi kwa Clatous Chama alipogoma kujiunga na kambi ya timu kule Uturuki. Msimu huu wana jambo la Kibu mkononi. Hapo usisahau kuna jambo la Aishi Manula ambalo mashabiki pia hawalielewi.

Huo ni kwa upande wa klabu. Lakini kuna upande wa mchezaji pia. Kuna watu wanaitwa mameneja au tuseme kuna watu wanasema wapo katika menejimenti ya mchezaji fulani. Hawa wanaamini kwamba kazi yao kubwa ipo katika kusimamia maslahi ya kifedha ya mchezaji. Basi. Wanakosea.

Miongoni mwa kazi zao ni kujitokeza hadharani na kuelezea hali fulani inayomkabili mchezaji katika maisha ya nje ya uwanja. Wao hawapaswi kuzungumzia afya ya mchezaji. Hilo ni la daktari wa timu. Hawapaswi kuzungumzia kukosekana kwa mchezaji kwa sababu ya kadi nyekundu au za njano.

Lakini wanaweza kujitokeza na kuzungumzia hali ya mchezaji katika masuala ya kifamilia au wakati mwingine kama kuna timu imeleta ofa mezani kwake. Mameneja wa wachezaji wetu huwa hawafanyi hivi. Wakati mwingine mteja wao anaweza kuwa anasemwa vibaya, lakini wanashindwa kumsaidia kwa sababu hawatoi ushirikiano juu ya taarifa zake.

Tuanze kufanya mambo kisasa kwa ajili ya mustakabali wa soka letu. Tujifunze umuhimu wa mawasiliano na taarifa kwa umma. Kama hauzibi pengo hilo inakuwa rahisi kwa wataalamu wa kueneza uvumi kufanya kazi yao na kuuua morali ya timu.

Kibu alipaswa kujulikana yuko wapi na anafanya nini. Kama akiendelea kucheza Simba tayari mashabiki wa Simba wataanza kuwa na wasiwasi na uzalendo wake kwa klabu kama ilivyokuwa wakati ule walipokuwa wanakabiliana na suala la Chama.

Related Posts