Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani akimkabidhi kadi ya Mpiga
Kura, Bi. Hanifa Chija mkazi wa Mtaa wa Boma Kata ya Kimobwa, Wilayani Kasulu mkoani Kigoma
baada ya kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura katika kituo cha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tarehe 21 Julai,
2024. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya
Kigoma, Katavi na Tabora limeanza Julai 20 na litafikia ukomo Julai 26 mwaka
huu.
**************
Zoezi la Uboreshaji la Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora limeingia siku
ya pili baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa kulizindua Julai 20,2024 katika uwanja wa Kawawa Mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani alipata fursa ya kukagua
baadhi ya vituo vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la mpiga Kura katika Wilaya
za Kasulu za Buhigwe mkoani Kigoma na kujionea hali ilivyo vituoni na mwitikio
wa watu katika vituo hivyo.
Akizungumzia uboreshaji huo,
Kailima alisema hadi kufikia jana tarehe
21 Julai 2024, hapakua na changamoto yeyote iliyojitokeza katika mikoa yote ya
Tabora, Kigoma na Katavi na wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha lakini pia kuboresha taarifa zao.
Aidha, Kailima alivipongeza
vyama kwa kuweka mawakala katika vituo vya uandikishaji na kuwataka mawakala
hao kusaidia utambuzi kwa watu wasio raia wa Tanzania ambao watafika kwaajili
ya kuandikishwa.
Kailima alitumia nafasi hiyo
kuwakumbusha wananchi kuwa sasa zimesalia siku tano kati ya saba zilizopangwa kuandikisha
wananchi katika mikoa hiyo ya Kigoma, Katavi na Tabora hivyo wananchi wazitumie
siku zilizobaki kujitokeza na kujiandikisha.
Amesema vyama vya siasa
vinawajibu wa kuwahimiza, wanachama,wapenzi na wafuasi wao kujitokeza kujiandikisha na kuboresha
taarifa zao ili waweze kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wananchi waliojitokeza kujiandikisha na wengine kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani (kulia) akiwa katika kituo cha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu.
Afisa mwendesha BVR, Sarah Malogo akimchukua alama za vidole Framk Laswai katika mfumo mwananchi aliyefika kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani (kushoto) akizungumza na baadhi ya maofisa uandikishaji katika Kituo cha Bohari ya Shule B Wilayani Kasulu.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika kituo cha Uboreshaji tayari kwa kuandikishwa na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani (kushoto) akishuhudia mwananchi akiandikshwa katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Mwananchi akiweka saini baada ya kukamilisha ujazaji wa fomu
Mwananchi akichukuliwa alama za vidole baada ya kukamilisha ujazaji wa fomu