Wakati taarifa zikienea kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis amekimbilia Norway, uongozi wa klabu hiyo umesema utamchukulia hatua za kinidhamu ikidai ni mtoro.
Kauli ya Simba inakuja baada ya kuibuka kwa taarifa Kibu ametimkia Norway kimya kimya bila kutoa taarifa kwa klabu yake.
Simba imezinasa nyaraka mbalimbali za Kibu zikionyesha kiungo huyo ametimka nchini na sasa inafanya mawasiliano na uongozi wa mchezaji huyo.
Sakata hilo limeibuka baada ya kiungo huyo kuzusha sintofahamu ya kutorejea kazini, tangu asaini mkataba mpya wa miaka miwili kisha kutimkia Marekani kwa mapumziko ya mwisho wa msimu.
Hata aliporejea nchini akitokea Marekani, Kibu hakujiunga na timu hiyo licha ya uongozi wa Simba kupitia Meneja wa Habari, Ahmed Ally kuthibitisha klabu yao imechukua hatua nyingi za kumsaka ili akajiunge na wenzake kwenye kambi yao iliyoko jijini Ismailia, Misri.
Simba kwa sasa iko Ismailia ilikoweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, huku mchezaji huyo hadi sasa bado hajaripoti na taarifa zinadai ametimkia Norway.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya klabu hiyo leo Julai 23 , imeeleza sababu za mchezaji huyo kitojiunga na kambi ya timu hiyo hadi sasa.
“Klabu ya Simba inautaarifu umma, mchezaji wake Kibu Denis Prosper hajaripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2024-2025.”
“Tunapenda kuutarifu umma, Simba tulimwongezea mkataba Kibu wa miaka miwili zaidi utakaoisha Juni 2026 na kumlipa stahiki zake zote za kimkataba,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza;
“Hata hivyo mchezaji huyu amekuwa akitoa sababu kadha wa kadha zinazomfanya kushindwa kuripoti kambini na kutokana na utovu huu wa nidhamu, klabu itamchukulia hatua stahiki za kinidhamu na umma utapewa taarifa,” mwisho wa kunukuu taarifa hiyo.