Kikwazo utekelezaji mikakati taasisi za umma chatajwa

Unguja. Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said amesema licha ya taasisi za Serikali kuandaa mikakati mizuri, inashindwa kutekelezwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo watendaji wengi kutokuwa na uelewa wa mipango hiyo.

Zena ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 22, 2024 wakati wa semina ya siku mbili ya makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, watendaji wakuu wa taasisi na maofisa wadhamini iliyoandaliwa na Taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Watendaji Serikalini (PDB).

Amesema kuna mambo mengi yanasababisha kufeli utekelezaji wa mipango hiyo, hasa ukosefu wa usawa kwa kuwa mtu asipojua anachotakiwa kufanya ni vigumu kukifanya.

Zena amesema kingine kinachokwamisha utekelezaji wa mipango hiyo ni kukosekana watu wa kutekeleza ilhali watendaji wapo ndani ya taasisi.

“Kila taasisi ina mipango mikakati yake, inaandaliwa bajeti kubwa kuiandaa, lakini wakati wa utekelezaji kuna tatizo kufikia malengo. Mara nyingi hakuna shida kwenye kutengeneza mikakati, lakini kuna shida kwenye utekelezaji kwa hiyo naamini tutapata kujua nini, na watu gani wahusika wakuu,” amesema.

Amesema wakati mwingine wanakuwa hawafanikiwi kwa sababu wanashindwa kupata usaidizi kutoka kwa wahusika wote katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Jambo lingine lililotajwa na kiongozi huyo ni hata unapofika wakati wa kupima vigezo vya utekelezaji wa mipango hiyo inafanyika ilmradi imefanyika.

“Kwa hiyo lazima tuhakikishe mikakati yetu tunayoiandaa inakuwa wazi na kueleweka na wote wanaotakiwa kuitekeleza,” amesema.

Amesema wakati mwingine watendaji wa chini hawajui mipango mikakati ya taasisi zao, badala yake inajulikana na menejimenti na bodi wanapomaliza kuitengeneza inafungiwa kwenye kabati.

“Ikimaliza kutengenezwa inabaki kwenye kabati, kwa hiyo watumishi wanakuwa hawajui mipango mkakati ipoje na wajibu wao kushiriki katika kuitekeleza hawajui ni nini. Tunakuwa na shida wakati mwingine kwa sababu hawajui cha kufanya,” amesema.

Ameeleza kama wanajua wakianza kutekeleza wanatakiwa kuona mchango wao ila wasipoona wataona kwamba hawana sababu ya kutekeleza mipango hiyo.

Changamoto nyingine inayotajwa na kiongozi huyo kukwamisha utekelezaji wa mipango hiyo ni kukosekana  mpangilio maalumu ndani ya taasisi husika, pia kukosekana rasilimali watu.

“Tuhakikishe kuna mpangilio, kukosekana kwake inakuwa chagamoto nyingine na lazima kuwepo na rasilimali watu, ili tusifeli lazima kuandaa utendaji kazi kwa kupimana,” amesema.

Amesema ukosefu wa mawasiliano unachangia pia katika utekelezaji wa mikakati yao.

“Lazima tuwe na mawasiliano mazuri na wadau wajue,” amesema.

Amewataka wakuu wa taasisi hizo wanapoteua watendaji kwenda kwenye mafunzo ya muda mrefu au mfupi kuhakikisha yanaleta tija badala ya kuteua watu kwa ajili ya kujiongezea kipato.

“Mtu haendi kujifunza kitu ila anakwenda ili aonekana leo kaenda fulani lakini tija yake inakuwa haionekani, yale mafunzo yanayofanyika kila mwaka lazima yalete tija na siyo kwa ajili ya watu kujiongezea kipato,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ushauri wa menejimenti ya Tanfidh kutoka Oman, Said Saif Alharthi amesema kuwa na mipango bila utekelezaji ni sawa na ndoto za mchana; lakini kutekeleza mipango ambayo haipo ni kupoteza muda.

Related Posts