Kuna Maxi Nzengeli mmoja tu Yanga

BEKI wa kushoto wa FC Augsburg, Mads Pedersen ambaye msimu uliopita wa mashindano Ujerumani alicheza michezo 27 ya Ligi Kuu (Bundesliga) na moja ya Kombe la DFB-Pokal, ameukubali mziki wa winga Mkongomani wa Yanga, Maxi Nzengeli katika mchezo wa kirafiki ambao timu hizo zilikutana katika michuano ya Mpumalanga Premiers huko Afrika Kusini, mwishoni mwa wiki.

Pedersen ambaye katika mchezo huo wa kirafiki alifunga bao la kwanza kwa Augsburg iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1, alimfuata Nzengeli kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga na kubadilishana naye jezi ikiwa ni ishara tosha ya kukubali uwezo wake.

Achana na asisti ambayo Nzengeli alitoa kwa Jean Baleke, ambaye alifunga bao la Yanga kwenye Uwanja wa Mbombela, ukubwa wa nishati ya mchezaji huyo na uwezo wa kutumika katika maeneo mengi ni kati ya mambo ambayo yamekuwa yakimbeba kwenye kikosi cha Wananchi.

Miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao msimu uliopita waliuanza vizuri kwa kuonekana mara kwa mara kwenye orodha ya wafungaji kila ambapo timu hiyo ilipokuwa ikiibuka na ushindi ilikuwa ni pamoja na Nzengeli, aliyeifungia mabao 11 katika ligi.

Tofauti na namna alivyouanza msimu uliopita kuna wakati Nzengeli alikuwa akiandamwa na ukame na hilo halikumfanya kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, kuacha endelea kumpa nafasi kati ya viungo watatu nyuma ya mshambuliaji wa mwisho. Unajua kwanini? Hicho ndicho kilichomfanya nyota wa Augsburg, Pedersen kubadilishana jezi na Mkongomani huyo.

Uwezo wa kuwa karibu katika kila eneo wakati wa kushambulia na hata kuzuia ni upekee ambao Nzengeli amekuwa nao katika kikosi cha Yanga ukimlinganisha na wachezaji wengine ambao wamekuwa wakicheza katika maeneo ya ushambuliaji kama vile Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua.

Kivipi? Mara nyingi Mkongomani huyo amekuwa akitumika kama mshambuliaji wa pembeni – inaweza kuwa winga ya kulia au kushoto, lakini amekuwa msaada wakati timu ikishambulia na kushambuliwa.

Nzengeli ni N’Golo Kante wa Yanga. Siyo aina ya wachezaji ambao huongelewa sana uwanjani, lakini mara nyingi amekuwa akifanya kazi kubwa, akikimbia muda wote wa mchezo kama ilivyo kwa kiungo huyo wa Kifaransa ambaye wapo mashabiki ambao wamekuwa wakitania wakisema asilimia 70 ya dunia imefunikwa na maji na iliyobaki ni mchezaji huyo. 

Zipo mechi ambazo kocha hutumia wachezaji kwa majukumu maalum, Nzengeli ni mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya kimbinu mfano mzuri tuliona msimu uliopita katika michezo miwili migumu kwa Yanga ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Tofauti na namna tulivyozoea kumwona akicheza kati ya viungo watatu washambuliaji, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alimua kuongeza nguvu katika eneo la mwisho la ushambuliaji kwa kuanza na Joseph Guede na Clement Mzize huku Mkongomani huyo akicheza kama beki wa kisasa wa pembeni ‘wing back’.

Yanga ilicheza mchezo huo bila ya kuwa na beki wa kulia asilia, Gamond alianza na mabeki watatu wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto ndani ya dakika 180 za michezo yote miwili ya robo fainali Mamelod Sundowns na Nzengeli alifanya vizuri.

Usajili wa Clatous Chama Yanga uliwafanya baadhi ya wadau wa soka la Tanzania kupanga kikosi cha timu hiyo ya Wananchi bila ya kumjumuisha Mkongomani huyo, ni kama wanamwona pengine anaweza kupotea.

Sio rahisi kwa Nzengeli kupotea kutokana na utofauti alionao, kitazame kikosi cha timu ya taifa la Ufaransa, ukianza kuongelea majina walinayo unaweza kuogopa lakini panga pangua Didier Deschamps amekuwa akimpa nafasi Kante na alikuwa msaada kwenye michuano ya Euro, Ujerumani.

Pacome, Chama na Aziz KI ni wachezaji wazuri ambao wanaweza kuurahisha mchezo kutokana na ufundi walionao lakini Nzengeli mbali na uwezo wa kushambulia alionao unaweza kuona umuhimu wake pia wakati timu ikishambuliwa kutokana na nishati aliyonayo.

Pamoja na yote hayo mwisho wa siku, Gamondi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho na kwa bahati nzuri aliweka wazi kuwa anachotazama ni uwajibikaji wa mchezaji na sio ukubwa wa jina lake hivyo Nzengeli, Pacome, Chama na Azizi KI wote wananafasi ya kuuwasha moto kwenye eneo la kiungo mshambuliaji ambalo ni kama uti wa mgongo wa Yanga. 

Kocha wa timu za vijana za Azam FC, Mohamed Badru amemzungumzia Nzengeli kama silaha ambayo itakuwa ikiangamiza kimyakimya huku akiweka wazi kuwa nyota huyo amekuwa akimvutia sana.

“Binafsi ni kati ya wachezaji wa kigeni ambao navutiwa nao, ni mchezaji wa kitimu zaidi, unaweza kumuona kila eneo kwa sababu anauwezo wa kufanya hivyo, hakuna mchezaji wa namna hiyo ambaye anaweza kukaa benchi, anasifa za kipekee,” anasema kocha huyo.

“Ni kweli kwamba Chama, Pacome ni Aziz KI ni wachezaji wazuri sana lakini katika mazingira ya timu ikiwa inaumiliki mkubwa wa mchezo, wote hao wanaweza kuwafungua wapinzani.Lakini ikiwa mnacheza na timu inayojua kutumia mianya mkiwa eneo lao yani wanaweza kushambulia nkwa kustukiza basi hilo ni janga.”

Related Posts