Mtoto adai kuunguzwa moto kisa Sh70,000

Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia John Matemi (48) kwa tuhuma za kumshambulia mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka 14 kwa viboko na kumuunguza mkono, akimtuhumu kumuibia Sh70,000.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumanne Julai 23, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema wanamshikilia John kwa tuhuma za kumshambulia mtoto huyo.

Amesema uchunguzi ukikamilika watamfikisha mtuhumiwa kwenye vyombo vya sheria kujibu shitaka litakalomkabili.

Akisimulia tukio hilo, mtoto huyo (jina linahifadhiwa) amedai tukio hilo lilitokea Jumapili, Julai 21, 2024, akiwa nyumbani kwa bibi yake.

Amedai mjomba wake alimtaka atoe Sh70,000 alizodai amemuibia kwenye suruali aliyokuwa ameitundika chumbani.

“Siku ya Ijumaa alikuja na mama yangu huku kwa bibi ambako nakaa tangu nikiwa mdogo. Nikaambiwa nikalale na mfanyakazi wa mjomba ambaye nyumba yao iko jirani na kwa bibi. “Jumamosi asubuhi, mfanyakazi aliwahi kuamka na akaniamsha na mimi kwenda shule,” amesimulia mtoto huyo.

Amesema alipokuwa shuleni, mama yake alimfuata na kumtaka atoe hela alizodai ameziiba kutoka kwenye mfuko wa suruali ya mjomba wake.

“Nilishangaa, nikamwambia mama sijachukua hela yoyote, lakini hakuniamini akaondoka. Jioni niliporudi mama alinichapa sana huku ananiambia nitoe hela nilizochukua kwa mjomba, lakini nilikataa sijachukua,” amesema.

Mtoto huyo amesema baada ya kipigo aliachiwa, lakini Jumapili asubuhi mjomba wake alifika nyumbani kwa bibi yake huku akifoka akidai arudishe fedha hizo.

Amesema aliendelea kukataa kwamba hajachukua hela hizo na wakati anazungumza hivyo, mjomba wake alimsukuma na kumpigiza getini na kuanza kumchapa kwa fimbo ya ufagio akimtaka atoe hela na baadaye akamuunguza moto.

“Nilizidi kumuomba msamaha kwa sababu sijachukua hela yake.”

Amesema mjomba wake hakutaka kuamini bali alimburuta hadi jikoni ambako bibi yake alikuwa akipika chakula, akamshika mkono na kuutumbukiza kwenye moto.

Amesema aliokolewa na shangazi yake aliyepiga kelele za kuomba msaada kwa majirani waliofika kumuokoa.

“Baada ya kusikia kelele hizo, mjomba alinitoa mkono kwenye moto na kuendelea kunipiga kabla ya watu kujaa na kuniachia, baadaye nilipelekwa hospitali na kupatiwa matibabu.”

Shangazi wa mtoto huyo, Gladness Emmanuel, amesema alifika nyumbani hapo baada ya kusikia kelele kwa muda na kukutana na tukio hilo.

“Kiukweli niliumia sana nikapiga kelele, watu wakaja kusaidia ndipo tukampeleka hospitalini akapata matibabu. Kesho yake mkono ulizidi kutoa maji na kuharibika, tulifungua jalada kituo cha polisi ili angalau mtoto apate msaada wa matibabu,” amesema Gladness.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba watetezi wa haki za watoto kuingilia kati suala hilo ili kumsaidia apate msaada wa matibabu na kukomesha vitendo hivyo.

Baba wa mtoto huyo, Rabiel Lazier amesema amepata taarifa za tukio hilo leo asubuhi akaamua kwenda kwa wakwe zake kushuhudia.

 “Kiukweli nilipoona kidonda kile nilichoka kabisa na kupata presha hivyo sijataka kuongea tena. Acha suala hilo lishughulikiwe kisheria,” amesema baba huyo.

Related Posts