BEKI Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amemalizana na FC Lupopo ya DR Congo ambapo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo msimu ujao.
Ninja ameiambia Mwanaspoti kuwa sababu kubwa ya kusaini FC Lupopo ni kuona fursa katika timu hiyo kucheza michuano ya kimataifa ambayo itamfanya aendelee kuonekana katika mataifa mbalimbali. Timu itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Zilikuwepo timu mbalimbali zilizokuwa zinahitaji huduma yangu kutoka ndani na nje, lakini hadi nasaini nimeangalia mambo mengi ya msingi,” amesema.
“Katika Ligi Kuu ya DR Congo FC Lupopo ilimaliza nafasi ya pili, hivyo itacheza michuaono ya kimataifa kwangu niliiona ni fursa kubwa ya kuonyesha kipaji changu kwa upana.”
Aliongeza, “nimesaini mkataba wa mwaka mmoja, kwani kwa sehemu nina uzoefu na ligi yao, kikubwa kwa sasa naweka nguvu katika kazi, ili niweze kuyatimiza malengo yangu.”
Msimu uliopita Ninja alikuwa na Klabu ya Lubumbashi nchini humo ambayo alisaini miaka miwili akitumika mmoja na akaamua kuuvunja uliokuwa umesalia akitaja sababu ni maslahi.
“Yalikuwa mambo ya maslahi yaliyonifanya nivunje mkataba na Lubumbashi, ila tuliachana kwa amani nikapewa barua yangu na ndio maana naendelea na maisha mengine,” amesema Ninja ambaye aliwahi kucheza kwa mkopo katika klabu ya La Galaxy ya Marekani.
Msimu wa 2024/25 utakuwa wa pili kwa Ninja kucheza nchini humo ambapo alisema Yanga hataisahau katika maisha yake kwani imemfungulia milango na kupata fursa za kucheza nje.
“Kwa mara ya kwanza nilienda kucheza Ligi ya Marekani katika klabu ya LA Galaxy. Nikarejea tena ndani ya klabu hiyo wakati nakwenda kujiunga na Lubumbashi nilitokea Yanga ingawa nilikuwa nimemaliza mkataba,” amesema.