OCS na wenzake sita kortini wakituhumiwa mauaji ya raia

Bukoba. Askari Polisi wanne akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Kata ya Goziba, Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, John Mweji na mgambo watatu wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuua Baraka Lucas.

Mwili wa Lucas (20) aliyekuwa mbeba dagaa wabichi Mwalo wa Kisiwa cha Goziba, ulipatikana ukielea Ziwa Victoria Juni 12, 2024 ikiwa ni siku nne kupita tangu adaiwe kukamatwa na polisi wa kituo hicho Juni 9, mwaka huu.

Ndugu zake baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwa ndugu yao na askari wa doria usiku wa manane, walikwenda kituoni bila kufanikiwa kumuona na baadaye Juni 12, 2024 ndipo mwili wake ulionekana kando ya Ziwa Victoria ukielea.

Hii ni kesi ya pili kuhusisha maofisa wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji baada ya ile ya inayoendelea Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, ikiwahusisha maofisa saba walioshitakiwa kwa kosa la kumuua mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis.

Washtakiwa hao saba ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) wa Mtwara, Mrakibu wa Polisi (SP) Gilbert Kalanje na aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi (OCS) cha Mtwara Charles Onyango aliyekuwa Mrakibu Msaidizi (ASP).

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia, Nicholaus Kisinza, mkaguzi msaidizi wa Polisi Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu zahanati ya polisi akiwa na cheo cha mkaguzi msaidizi, Shirazi Mkupa na mshitakiwa Koplo Salum Juma Mbalu.

Washtakiwa wa kesi ya mauaji ya Baraka Lucas (20) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba kwa ajili ya kusikiliza kesi inayowakabili.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia, wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo wilaya ya Mtwara Januari 5, 2022 na kutupa mwili wake Majengo kata ya Hiari.

 Katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili OCS, John Mweji, washitakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba leo Jumanne Julai 23, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Masesa, huku polisi wakijaribu kuifanya kesi kuwa siri.

Hali hiyo ndiyo iliwapa wakati mgumu wanahabari kuweza kufahamu nani ni mgambo nani askari wa Jeshi la Polisi zaidi ya kuambiwa kuwa katika washitakiwa hao saba, Askari Polisi ni wanne na askari wa Jeshi la Akiba (mgambo) ni watatu.

Washtakiwa wengine mbali na OCS wametajwa kuwa ni Ahmad Rashid, Fransis Hayshi, Ally Jumanne, Emmanuel Massatu, Evodius Makaka na Athumani Malindo na watatu ni Polisi na watatu ni mgambo.

Akisoma shitaka hilo katika kesi hiyo ya mauaji (PI) namba 18914 ya mwaka 2024, Wakili wa Serikali, Agness Owino alidai kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 9, 2024 na hawakutakiwa kujibu lolote na kupelekwa mahabusu gerezani.

Hii ni kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo kusikiliza kesi za mauaji huku upande wa mashitaka ukiieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6, 2024 itakapotajwa tena.

Related Posts