Samaki aina ya papa wanaovuliwa kwa wingi katika pwani ya Brazili wamepimwa na kukutwa misuli na maini yao yakiwa na dawa ya kulevya aina ya kokeini (cocaine), wanasayansi wamesema.
Wanabiolojia wa baharini waliwapima papa 13 waliovuliwa pwani, karibu na Mji Mkuu Rio de Janeiro na walipowapima ndipo wakagundua wakiwa na viwango vya juu vya kokeini kwenye misuli na maini.
Viwango hivyo vilikuwa ni mara 100 zaidi ya vilivyoripotiwa hapo awali kwa viumbe wengine wa majini. Utafiti huo uliofanywa na Wakfu wa Oswaldo Cruz, ni wa kwanza kuonesha uwepo wa kokeini kwenye samaki hao aina ya papa.
Wataalamu wanaamini kuwa kokeini inaingia majini kupitia maabara haramu katika maeneo mbayo dawa hizo zinatengenezwa au kupitia kinyesi cha watumiaji wa dawa za kulevya.
Pakiti za kokeini zilizopotea au kutupwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya baharini pia zinaweza kuwa chanzo, watafiti wanasema.
Sara Novais, mtaalamu wa masuala ya sumu kutoka Kituo cha Sayansi ya Bahari na Mazingira cha Chuo Kikuu cha Leiria, ameliambia jarida la Sayansi kwamba matokeo hayo ni “muhimu na yanaonesha hali ya wasiwasi mintarafu afya za watu.”
Papa majike yote katika utafiti huo yalikuwa na mayai lakini matokeo ya kuathiriwa kwa vifaranga watakaozaliwa na kokeini bado hayajulikani, wataalamu wanasema.
Chanzo: BBC