Dodoma. Jeshi la Polisi limetoa taarifa kuhusu matukio ya miili ya wanawake wawili kuokotwa katika Kata ya Mkonze jijini Dodoma, likiwataka waliopotelewa na ndugu kujitokeza kuutambua mmoja.
Mwili huo ni wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30 uliopatikana kwenye korongo katika Mtaa wa Miganga, kata ya Mkonze Jumapili Julai 21, 2024 ukiwa umefungwa kwenye nailoni, boksi na kiroba.
Mwili mwingine ulipatikana Jumatatu Julai 22, 2024, karibu na mlango wa nyumbani kwake, Mtaa Chinyika ambao umetambuliwa kuwa ni wa Alice Ndondo (35).
Akizungumzia matukio hayo leo Julai 23, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya amesema Julai 22 Polisi walipatiwa taarifa kuhusu kuonekana mwili wa Alice nyumbani kwake mtaa wa Chinyika.
Amesema baada ya kufika eneo hilo, waliuchukua mwili huo na kuupeleka hospitali ambako daktari aliyeuchunguza aligundua kuwa ni kifo cha kawaida.
“Daktari aligundua alikufa kifo cha kawaida siyo kwamba alikuwa ameuawa. Kwa hiyo issue (jambo) ya Alice ni kifo cha kawaida karibu na nyumbani kwake,” amesema.
Kuhusu maelezo ya ndugu kwamba Alice alipotea kwa zaidi ya wiki nne lakini mwili ukapatikana nje ya nyumbani kwake, Kamanda Mallya amesema alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamume ambapo kuna wakati alikuwa akienda kuishi huko.
“Wakati mwingine alikuwa akiishi kwa mama mzazi na kwa huyu bwana. Ndiyo maana watu walikuwa wakifikiri labda atakuwa ameuawa na kutupwa katika nyumba hiyo.”
“Sisi tunategemea taarifa za daktari ambaye anatuambia kweli huyu mtu amekufa na chanzo cha kifo ni nini. Kama mtu ameuawa basi wanatuambia, kama ni kifo cha kawaida wanatuambia kama ilivyokuwa kwa huyu aliyekutwa nje nyumbani kwake,” amesema.
Kuhusu mwili mwingine ambao hadi sasa haujatambuliwa amesema:
“Mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wananchi wote wa eneo linalozunguka pale (alipookotwa) hawamfahamu. Kwa hiyo tunatoa wito kwa mtu yeyote aliyepotelewa na binti yake mwenye umri huo afike hospitali kwa upo hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi,” amesema.
Kamanda Mallya amesema kwa mtazamo wa awali, mwili wa mwanamke huyo haukuwa na majeraha isipokuwa ulikuwa ukitoka damu puani na mdomoni.
“Ili postmortem (uchunguzi wa kitabibu) ufanyike inahitajika kuwapo ndugu ili washuhudie. Ndiyo maana nimesema kama kuna mtu ambaye amepotelewa na ndugu yake anaweza kufika. Sasa hao ndio watasema kama wanataka mwili uchunguzwe au wameridhika na kifo chake,” amesema.
Amesema iwapo daktari akisema ameuawa ndipo uchunguzi wa tukio hilo (kuuawa) unafanyika.
Jana Julai 22, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Samwel Magesa alisema Julai 21, 2024, saa 11 jioni walipokea mwili wa mwanamke ambaye jina lake halikufahamika uliokuwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
“Alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, ilionekana baadhi ya majeraha kidogo yalikuwa yameenda ndani. Sehemu za kichwa pia zilikuwa na majeraha,” alisema.
Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Chinyika, Aloyce Maswikwi amesema mwili wa Alice utazikwa leo katika makaburi ya Shuleni yaliyopo Kata ya Mkonze.