PUMZI YA MOTO: Matokeo ya Kagame uthibibitisho Simba, Yanga, Azam zilikuwa sahihi

TIMU za Bara zilizoshiriki makala ya 44 ya Kombe la Kagame iliyofahamika kama Dar Port Cecafa Kagame Cup 2024 zimeshindwa kuvuka hatua ya makundi. Haikutarajiwa kuwaona wakiwa mabingwa, lakini wangeonyesha ushindani wenye kulingana na ubora wa ligi wanayotoka.

Ligi Kuu Bara ambayo ni ya sita kwa ubora Afrika ingedhihirisha ubora wake wa timu zake kufanya vizuri kwenye haya mashindano, lakini ikawa tofauti.

Costal Union ambao walikuwa na msimu bora sana wa 2023/24, hawakucheza kwa ule ubora wao waliokuwa na kuambulia nafasi ya pili kwenye kundi ambalo kwenye makaratasi lilikuwa jepesi sana kwao.

Timu          MP   W      D      L       GF   GA    Pts

Al-Wadi      3       2        1        0        4        2        7

Coastal      3       1        1        1        2        3        4

JKU             3       1        0        2        3        3        3

Dekedaha   3       1        0        2        3        4        3

Coastal Union ambayo kwenye ligi kuu msimu iliopita ilikuwa timu ya pili kwa kuwa na safu bora ya ulinzi, kwenye mashindano haya imekuwa pili ya pili kwa kuwa na safu mbovu zaidi ya ulinzi.

Mtu angetarajia kuona Coastal Union wakisherehekea kurudi kwenye mashindano haya ambayo mara ya mwisho kushiriki ilikuwa 1991 pale mashindano yalipofanyika Tanzania katika vituo viwili, Dar es Salaam na Tanga.

Coastal Union walipangwa kituo cha Tanga na wakafuzu nusu fainali kwa kuongoza kundi. Mpango wa awali wa Cecafa na FAT (sasa TFF) kama waandaazi wa mashindano ulikuwa mshindi wa kila kituo anabaki kituoni kumsubiri mshindi wa pili wa kituo kingine.

Kwa hiyo Coastal Union walitakiwa kubaki Tanga kumsubiri mshindi wa pili wa kituo cha Dar es Salaam, Nakibubo Villa Sports Club, ambayo sasa ni SC Villa ya Uganda.

Lakini Cecafa na FAT wakabadili kanuni na kusema kituo cha Tanga kinavunjwa na timu zote ziende Dar es Salaam.

Coastal Union wakagoma na kujitoa mashindanoni. Hii ilikuwa Coastal Union ya akina Juma Mgunda, ambaye alikuwa nahodha. Miaka zaidi ya 30 imepita, Coastal Union wamerudi kinyonge sana.

SINGIDA BLACK STARS – KUNDI C

Singida Black Stars ni timu inayojioambanua na kuwa tishio msimu ujao wa Ligi Kuu.

Aina ya wachezaji iliowasajili na ubora wa benchi lao la ufundi unadhihirisha hilo.

Lakini kwenye mashindano ya Kagame Cup 2024, wamemaliza kundi lao katika nafasi ya tatu wakiwa na safu mbovu zaidi ya ulinzi kwenye kundi.

Team                      Pld    W       D     L       GF    GA    Pts

 APR                          3        2        1        0        3        1        7

SC Villa                     3        1        2        0        4        2        5

Singida BS                3        1        0        2        4        5        3

Al-Merreikh Bentiu    3        0        1        2        1        4        1

Unaweza ukasema is alikuwa kundi gumu kwa kuwangalia wapinzani wao wawili wa juu, APR na SC Villa, lakini hata hivyo, hii haikuwa sababu ya kuruhusu mabao matano kwenye mechi tatu.

Hizi timu zingeweza kufanya vizuri zaidi ya walivyofanya, lakini tatizo kubwa ni kwam-ba hazikujiandaa.

Hiki ni kipindi cha maandalizi ya msimu mpya na kwa kawaida timu hutakiwa kufanya mazoezi angalau kwa wiki nne ili ziwe kwenye nafasi nzuri ya kushindana.

Na hiki ndicho walichokilalamikia Azam FC, Yanga na Simba, kiasi cha kushindwa kushiriki.

Msimu  wa mashindano wa 2023/24 uliisha kwa fainali ya Kombe la Shirikisho, Juni 2, 2024. Wachezaji walitakiwa wapate mwezi mmoja wa kupumzika kabla ya kurudi kwenye mikikimikiki ya msimu mpya wa 2024/25.

Mwezi wa kupumzika ni Juni na Julai warudi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Huo mwezi wa maandalizi ndiyo CECAFA wakaweka mashindano yao.

Kiufundi isingewezekana kwa timu zenye malengo makubwa kwa msimu mpya ku-shiriki mashindano haya kwa sababu nyingi sana. Utachezaje mashindano bila kujiandaa? Huyo mchezaji nguvu za kushindana atazipata wapi?

Timu zimetoka kusajili wachezaji wapya, saa ngapi wamezoeana na kuweza kucheza kama timu? Hiki ndicho Azam FC, Simba na Yanga walikikataa. Mashindano wanayaheshimu lakini siyo kwa ratiba hii.

Lakini Coastal Union na Singida Black Stars wakaona acha wajaribu kama watapata chochote, lakini mashindano hayana kujaribu, ni kushindana…na kama hukujiandaa vizuri utajulikana. Safari ijayo Cecafa ijitahidi kutafuta muda sahihi wa haya mashindano.

Cecafa ni chombo kinachounganisha vyama vyote za soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Iongee na vyama hivyo ili vibadili kalenda zao za mashindano.

Kila nchi ianze msimu mpya Septemba, ili Agosti uwe mwezi wa Kagame Cup.

Hii itasaidia kuondoka migongano, kama ilivyo kwa Mapinduzi Cup.

Zamani kulikuwa na migongano na malumbano baina ya TFF ikishirikiana na bodi ya ligi na timu za bara dhidi ya waandaaji. Lakini baadaye suluhisho likapatikana, mashindano yakawekwa kwenye kalenda rasmi ya pande zote za nchi yetu…sasa mambo ni shwari.

Na CECAFA wafanye hivyo, Agosti itachangamka na timu zetu zinaweza kuyatumia mashindano haya kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya Afrika.

Related Posts