MIAMBA ya soka la Ukraine, FC Shakhtar Donetsk imeachana na mpango wa kumsajili jumla nyota wa kimataifa kutoka Tanzania, Novatus Dismas aliyekuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea SV Zulte Waregem ya Ubelgiji.
Novatus ambaye mkataba wake na SV Zulte Waregem utatamatika Juni 30, 2025 ameonekana kutokuwa kwenye mipango ya kocha Marino Pusic licha ya kwamba mkopo wake ulikuwa na kipengele cha kusajiliwa jumla.
Pamoja na kwamba maisha yake yalianza vizuri huko Ukraine akiwa na Shakhtar Donetsk kwa kupata nafasi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto katika hatua ya makundi, ghafla kibao kiligeuka na kujikuta akipoteza nafasi.
Kocha wa Shakhtar, Pusic alipendelea zaidi kumtumia Valeriy Bondar na Mykola Matviienko kati ya mabeki wake wa kati huku kushoto akicheza Irakli Azarovi maeneo ambayo Novatus amekuwa akiyamudu.
Katika dirisha hili la usajili, Pusic ameongeza nguvu eneo ambalo Novatus alikuwa akipigania namba kwa kusajili beki kutoka CS Sfaxien ya Tunisia, Alaa Ghram huku akipandishwa Roman Savchenko ambaye naye ni beki wa kati kutoka kikosi B cha chama hilo.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa Novatus inaelezwa kwamba mchezaji huyo anasikilizia uwezekano wa kutoka tena kwa mkopo.
“Anatamani kupata fursa sehemu nyingine ili endelee kupambania ndoto zake, bado haijafahamika kama atasalia SV Zulte Waregem au laa,” alisema rafiki huyo ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi.