SMZ yatoa angalizo mawakala feki elimu ya juu

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kumekuwapo na wimbi la mawakala feki wanaowaliza wazazi na wanafunzi wakidai kuwapeleka kusoma vyuo vya elimu ya juu nje ya nchi kumbe hawana sifa, hivyo kuwataka wajihadhari na utapeli huo.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (Wema), Abdugulam Hussein amesema hayo leo Julai 21, 2024 alipofunga maonyesho ya Wiki ya Elimu ya Juu yalioanza Julai 15, 2024.

Naibu Waziri Abdugulam amesema wapo wazazi wengi wamelizwa na mawakala ambao hawajasajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), hivyo mbali na kupoteza gharama nyingi, pia wanapoteza muda na vyeti vyao wanaporejea nchini vinakuwa havitambuliki na Serikali.

“Wazazi mnao wajibu wa kushirikiana na wizara kuwatambua mawakala waliosajiliwa, kumekuwa na tabia kuibuka watu wengi kusafirisha vijana nje ya nchi lakini hawana sifa, kwa hiyo tuendelee kushirikiana na Serikali kuepuka watu wa namna hiyo,” amesema.

“Wizara tunaotoa tahadhari na kuwaonya wanaojifanya mawakala kumbe siyo wakweli na tutachukua hatua za kisheria,” amesema.

Amesema baadhi ya mawakala wanawapeleka wanafunzi katika vyuo ambavyo havitambuliki ikifika hatua ya mwisho wanakuwa wameshatumia gharama kubwa, muda mwingi lakini vyeti vyao wanaporejea nchini vinakuwa havitambuliki.

Hata hivyo, amesema iwapo kuna watu wanakumbana na changamoto hiyo watoe taarifa ili watu hao washughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Akizungumzia maonyesho hayo amesema yamekwenda na wakati kwani kwa sasa vyuo vimeshaanza udahili, huku bodi ya mikopo  ikianza usajili wa wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo.

“Imani yetu kama wizara maonyesho haya yamekwenda vizuri lakini kasoro ambazo zimejitokeza tunaahidi kuzishghulikia ili maonyesho yanaokuja yawe na ufanisi mkubwa zaidi,” amesema.

Mkuu wa kitengo cha uratibu wa elimu ya juu, Aida Maulid bila kutaja takwimu kamili, amesema idadi ya waliotembelea maonyesho hayo imeongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka iliyopita.

Baadhi ya wanafunzi waliofika katika maonyesho hayo wamesema utaratibu huo unawarahisishia kwa kuwa wanapata ushauri na kujisajili haraka tofauti na kwenda kwenye vyuo husika.

“Binafsi nimefanya usajili hapa wa bodi ya mkopo, lakini nimepata ushauri wa kozi nzuri za kusoma kwa hiyo kila kitu nimeshakamilisha kilichobaki ni kwenda masomoni,” amesema Ashura Said Mwinyi.

Related Posts