Dar es Salaam. Kutokana na ubunifu na umahiri katika kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja na wadau wengine, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya Benki Bora Tanzania inayohudumia biashara ndogo na za kati kwa mwaka 2024.
Tuzo hiyo imetolewa na Jarida la Euromoney la nchini Uingereza ambalo hutambua benki na taasisi za fedha zenye mchango mkubwa kwa jamii inazozihudumia.
Mkurugenzi wa Biashara ya Awali na Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul akipokea tuzo hiyo amesema wameongeza juhudi katika kuwahudumia wajasiriamali nchini kwa kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji yao.
Miongoni mwa hizo amesema ni utaratibu wa kuwaruhusu wajasiriamali kukopa kwa kutumia taarifa za mtiririko wao wa mzunguko wa fedha za biashara bila kuhitaji dhamana.
“Mfanyabiashara mwenye hati ya ununuzi anaweza kupata mkopo kutoka CRDB. Tunashirikiana na wadau tofauti kufanikisha hili,” amesema.
Amesema mwaka 2023, ilikopesha zaidi ya Sh8.9 trilioni na asilimia 12 ya kiasi hicho kilielekezwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Paul amesema matumizi ya teknolojia hasa katika malipo yameongeza ufanisi katika biashara za wajasiriamali wengi.
Ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, Paul amesema benki imetanua wigo kwa kuwahusisha wafanyabiashara wachanga ambao hunufaika kwa mafunzo na elimu ya fedha inayotolewa kupitia majukwaa tofauti.
Amesema mkakati wa muda wa kati wa miaka mitano (2023 -2027), umetoa kipaumbele katika uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo, na kati (MSMEs).
Paul amesema katika nusu ya mwaka huu tayari CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya jumla ya takribani Sh1.5 trilioni.