Afisa mmoja katika ofisi ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba ujumbe wa ngazi ya juu kutoka serikali ya Kongo na ule wa muungano wa makundi ya wapiganaji wa M23 na AFC wanakutana mjini Kampala kujadili njia za kuleta amani nchini Kongo.
Kuundwa kwa AFC, au Alliance Fleuve Congo, inayoyaleta pamoja makundi kadhaa ya waasi, ulitangazwa mwezi Disemba na Corneille Nangaa, mkuu wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Kongo, ambaye anaishi uhamishoni nchini Kenya. Afisa huyo wa Uganda alisema Museveni pia atashiriki katika mazungumzo hayo pamoja na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye amekuwa mpatanishi katika mzozo huo kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Uganda inaongoza mazungumzo ya amani kati ya pande zinazohasimiana Kongo
Katika siku za nyuma, Kenya na Angola zote zimeshiriki kama wapatanishi katika mazungumzo ya amani kati ya pande zinazozozana. Afisa huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa kwasababu ya kukosa idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari, amesema kutokana na utata uliopo, mkutano huo ni wa siri lakini maelezo yatawekwa wazi baadaye.
Chanzo hicho pia kimesema kuwa nia yao ni usitishaji vita wa kudumu na amani kurejea nchini Kongo. Chanzo kingine ndani ya M23 kilithibitisha mazungumzo hayo lakini kilisema bado hayajaanza na kwamba kile anachofahamu ni kwamba waliitwa tu mjini Kampala.
Hata hivyo, kupitia mtandao wa X, waziri wa mawasiliano wa Kongo ambaye pia ni msemaji wa serikali Patrick Muyaya, alisema kuwa hakuna mtu aliyepewa mamlaka na serikali kwa majadiliano yoyote kama hayo na magaidi wa RDF (Jeshi la Ulinzi la Rwanda) au M23 mjini Kampala.
DRC yakanusha kuendelea kwa mazungumzo ya aina yoyote na waasi wa M23
Jean Bosco Bahala, mratibu wa Mpango wa Kuondoa Silaha, Kuokoa Jamii na Uimarishaji (P-DDRCS) nchini Kongo, amesema kwa sasa yuko Kampala lakini pia amekanusha kuhusu mazungumzo yoyote yanayoendelea na kundi la M23.
Akiwa mjini Goma, Bahama aliiambia AFP kwamba suala la majadiliano na M23 ni la uongo na kwamba mpango wa P-DDRCS uko kwenye majadiliano na Uganda kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani watoto wa Kongo walioachiliwa na kundi la Lord’s Resistance Army (LRA) katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kundi hilo la LRA lilianzisha uasi dhidi ya Museveni mnamo mwaka 1986, na kuua zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 katika uongozi wa muongo mmoja ulioghubikwa na vitisho vilivyoenea hadi Sudan, Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Nyongeza ya muda wa kusitisha mapigano yaheshimiwa Kongo
Wiki iliyopita, serikali ya Kongo ilimuita mkuu wa ujumbe wa kidiplomasia wa Uganda nchini Kongo kufuatia ripoti ya wataalamu iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, iliyosema kuwa Kampala ilikuwa inatoa msaada kwa M23.
Naibu msemaji wa wizara ya ulinzi ya Uganda Deo Akiiki, alitaja madai hayo kuwa ya kuchekesha na yasiokuwa na msingi .
Ripoti hiyo ya wataalamu pia ilisema kuwa wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wamekuwa wakipigana pamoja na waasi wa M23 katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini na kwamba Kigali ina “udhibiti wa ukweli” wa operesheni za kundi hilo. Rais wa Rwanda Paul Kagame hajakanusha waziwazi uwepo wa majeshi ya Rwanda nchini Kongo, lakini hajaonekana akitetereka juu ya nia yake ya kulinda maslahi ya nchi yake.