Umasikini, malezi chanzo cha matukio ya uhamiaji usiofuata taratibu

Dar es Salaam. Matamanio ya kuwa na maisha mazuri ni moja ya sababu za kushamiri vitendo vya uhamiaji usiofuata taratibu na biashara haramu ya usafirishaji binadamu.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Julai 23, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abeida Rashid katika mdahalo wa kitaifa uliojadili masuala ya uhamiaji ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IMO).

Amesema baadhi ya watu wamejikuta wakiingia katika vitendo hivyo kutokana na kuamini watakwenda kupata maisha mazuri bila kufikiria athari wanazoweza kukumbana nazo.

Katibu mkuu huyo amebainisha makundi yanayoathirika zaidi na vitendo hivyo ni wanawake na watoto.

Ameeleza upande wa watoto kinachochangia kufanya vitendo vya uhamiaji usiofuata taratibu ni pamoja na wazazi kutozingatia malezi bora na ukatili ndani ya familia.

Kwa upande wa Zanzibar amesema wana nyumba maalumu zinazojulikana ‘nyumba salama’ ambazo lengo lake ni kuwahifadhi waathirika wa uhamiaji usiofuata taratibu wakati wakisubiri kuunganishwa na familia zao.

Amesema mwaka jana walipokea watoto 61 na mwaka huu hadi kufikia Julai wamepokea watoto 19 wote wakitokea Tanzania Bara.

“Wanapokuwa katika nyumba hizo hufundishwa stadi mbalimbali ili watakapokutanishwa na familia wawe tayari na ujuzi utakaoweza kuwasaidia,” amesema.

Rashid amesema matukio hayo siyo tu yanaleta athari za kijamii kwa familia kusambaratika lakini pia kiuchumi kutokana na kuhitajika kuwekwa fungu la fedha kwa ajili ya kuwahudumia.

Amesema ili kutokomeza vitendo hivyo kuna haja ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa wanajamii kuhusu athari zake.

Awali, Mkuu wa Ofisi ya Msimamizi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Shabnam Mallick, ameainisha takwimu za Umoja wa Mataifa zinazoonyesha kuwapo wahamiaji kimataifa milioni 281 sawa na asilimia 3.6 ya idadi ya watu duniani.

Kamishna Mwandamizi wa Uhamiaji, Thomas Fussy amesema Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo ina mpaka mkubwa unaozungukwa na nchi takribani nane zikiwamo Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia Demokrasia ya Congo (DRC).

Amesema hilo linasababisha mwingiliano na watu wa mataifa hayo, ambao huja kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kibiashara na machafuko ya kisiasa.

Fussy amesema Tanzania imeendelea kuimarisha ulinzi katika mipaka yake na kuhakikisha wanaoingia nchini wana vibali vya kufanya hivyo.

Ofisa Mradi Msaidizi kutoka IMO, Ken Heriel amesema uwepo wa midahalo kama hiyo inayokutanisha wadau wa masuala ya uhamiaji ni muhimu kwa kuwa inasaidia kufahamu hali halisi ilivyo na nini kinapaswa kufanyika.

Related Posts