Wademocrat wajitokeza kumuunga mkono Harris – DW – 22.07.2024

Wachambuzi wanasema kampeni za Harris zinatakiwa kwenda mbali zaidi ya kujikita katika kupambana na mpinzani wake kupitia chama cha Republican, Donald Trump. 

Makamu wa Rais Kamala Harris tayari ameanza kuwashawishi wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha Democratic kumuunga mkono anapoianza safari ya kuelekea White House baada ya Rais Joe Biden kujiengua jana Jumapili.

Ikiwa atafanikiwa kupeperusha bendera ya Democratic, Harris atatakiwa kuchagua mgombea mwenza na kuanzisha operesheni kubwa ya kisiasa ili kuimarisha ushawishi wake, zikiwa zimesalia siku 100 tu hadi kufanyika uchaguzi mkuu.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni uungwaji mkono mkubwa, Harris aliidhinishwa mara moja na viongozi wa makundi kadhaa yenye ushawishi na hata ya kisiasa ambayo ni pamoja na Wakfu wa Ushindi wa AAPI, unaojihusisha na wapiga kura wa asili ya Asia na Pasifiki, The Collective PAC, unaojikita katika kuimarisha nguvu ya kisiasa kwa watu weusi pamoja na Wakfu wa Ushindi wa Amerika ya Kusini, miongoni mwa mengineyo.

Soma pia: Baada ya Biden kujiengua, Kamala Harris aanza kuupigania urais 

Urusi tayari imeonyesha mashaka kuhusiana na uwezekano wa Harris kugombea urais, ikisema hajakuwa na mchango wowote mkubwa katika uhusiano na Moscow, zaidi ya kutoa matamshi makali na yasiyo ya kirafiki.

Urusi | Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov amesema hawawezi kutoa tathmini yoyote ya ugombea wa urais wa Kamala Harris kutokana na uhusiano tete baina ya mataifa hayo Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari alipoulizwa kuhusiana na uteuzi wake kwamba matukio ya Marekani dhidi ya Moscow katika siku za karibuni yanawafanya wasishangazwe na chochote kinachofanywa na taifa hilo.

“Kwa sasa hatuwezi kutathmini kuhusu ugombea wa Harris kwa mtizamo wa uhusiano baina yetu. Kwa sababu hadi sasa, hatujaona chochote alichochangia kwenye uhusiano huu,” alisema Peskov.

Aliyewahi kuwa mshauri wa masuala ya kimkakati kwenye kampeni za Barack Obama Julius van de Laar ameiambia DW kwamba, Harris anatakiwa kwenda mbali zaidi kwenye kampeni zake, badala ya kuangazia tu namna ya kumdhibiti Trump. Amesema kwa kuwa Republican walikuwa wakitumia umri wa Biden kama kigezo cha kutofaa kuongoza, sasa ni zamu ya Harris mwenye miaka 59 tu kutumia kibao hichohicho kumtandikia Trump.

Soma pia: Uchaguzi wa Marekani: Rais Joe Biden ampisha Kamala Harris

Hata hivyo, amesema atalazimika kwenda mbali zaidi kwa kuelezea maono yake ya siku za usoni na kuwa na ujumbe utakaobadilisha mitizamo ya wapiga kura na, zaidi, kuleta tofauti kubwa kutoka huko walikotoka na wanakoelekea.

Baadhi ya wagombea wenza wanaotajwa ni Gavana wa Pennysylvania Josh Shapiro, Gavana wa North Carolina Roy Cooper na Seneta wa Arizona Mark Kelly.

Ikiwa atachaguliwa, Kamala Harris atakuwa sio tu mwanamke wa kwanza bali pia mwanasiasa wa kwanza mwenye asili ya Asia Kusini kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani.

Soma pia: Biden ampendekeza Harris baada ya kujiondoa mbioni

Related Posts