Dar es Salaam. Kupanda bei za bidhaa, utitiri wa kodi, tozo, ushuru na mazingira magumu ya kujipatia kipato ni mambo ambayo Chama cha ACT-Wazalendo kimeeleza kusikitishwa nayo kutokana na namna wananchi wanavyoumia.
Viongozi wa chama hicho wameeleza hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano waliyoifanya katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Simiyu, Kigoma na Ruvuma wakiwa kwenye ziara iliyoanza Julai 22, 2024.
Kwa mujibu wa viongozi hao, hawaoni jitihada zinazofanywa na Serikali kutatua suala la ugumu wa maisha ya wananchi.
Akiwa Kondoa mjini, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema kupanda kwa gharama za maisha kumeathiri uwezo wa wananchi kupata mahitaji ya msingi.
“Tunaona bei za mafuta ya petroli na dizeli kwa miaka mitatu zimepaa kutoka wastani wa Sh2, 040 kwa lita mwaka 2021 hadi kufikia Sh3,270 mkoani Dodoma. Nauli za mabasi zimepanda, mbolea nazo hazikamatiki, ruzuku kwenye mbolea haiwafikii wakulima,” amesema Semu.
Amesema gharama kubwa za maisha zinawaingiza wananchi kwenye umasikini kwa sababu wanashindwa kununua chakula, kugharimia afya, maji na umeme.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Isihaka Mchinjita amesema wananchi wa Ruvuma wanapitia ugumu wa maisha kutokana na kupanda bei ya mbolea tangu mwaka 2021.
Amesema usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima hauwanufaishi walio wengi, hivyo kushindwa kuzalisha na hatimaye kuingia katika umasikini.
“Tunafahamu kilio chenu kikubwa ni kuona mnaweza kupata mbolea kwa wakati, kwa bei nafuu na yenye ubora. Serikali ya CCM inawahadaa kuwa inaweka ruzuku lakini wengi wenu hamjapata mbolea ya ruzuku. Mwaka huu hali ni mbaya zaidi, gharama za uzalishaji zimekuwa juu na bei ya mahindi imezidi kuporomoka,” amesema Mchinjita.
Amesema wananchi hawapaswi kuendelea kushuhudia maisha yao yakigandamizwa na viongozi wasiojali.
Wilayani Busega, mkoani Simiyu, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema kuporomoka kwa bei ya pamba, kutoka Sh2,000 kwa kilo mwaka 2022 mpaka kuuzwa Sh1,060 mwaka jana kumeongeza maumivu na hali ngumu ya maisha.
Kwa upande wake, kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe akiwa mkoani Kigoma amesema asilimia 30 ya wananchi kutoka mikoa saba ya Tanzania wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
“Hii inamaanisha hawana uwezo wa kupata na kutumia Sh1, 700 kila siku. Mikoa hii tumeiita mikoa ya ukanda wa umasikini – Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Shinyanga, Kagera na Geita,” amesema Zitto.