Benki ya Maendeleo yavuka kizingiti, sasa kutoa huduma nchi nzima

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo imesema sasa itafanya kazi nchi nzima tofauti na awali ambapo uwezo wake ulikuwa unaishia kwenye kanda.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufikisha mtaji wa Sh19 bilioni kutoka Sh17 bilioni za mwaka 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24,2024 Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo, Peter Tarimo amesema tayari imepata kibali cha Benki Kuu (BoT) kinachoruhusu kufanya kazi nchi nzima.

“Mafanikio haya yalisubiriwa kwa hamu kubwa kwa miaka mingi kutokana na kigezo cha mtaji ambapo benki ilikuwa na hadhi ya kikanda. Kwa sasa benki imefikisha mtaji wa bilioni 19 ambao unakidhi kuiwezesha kufanya kazi kote nchini,” amesema Tarimo.

Amesema ukuaji huo wa faida ulichangiwa zaidi na mikakati ambayo benki imejiwekea pamoja na ushirikiano kutoka kwa wateja na wadau mbalimbali.

Pia amesema faida ya benki imeongezeka kutoka Sh1.4 bilioni mwaka 2022 hadi Sh2.35 bilioni mwaka 2023, hatua inayoiwezesha kutenga gawio la Sh1.17 bilioni, sawa na Sh44 kwa kila hisa.

Tarimo amesema benki imejiwekea sera ya ugawaji wa sehemu ya faida kwa wanahisa ambapo hutoa asilimia 50 ya faida.

“Mkutano mkuu ulipendekeza gawio liwe kwa mfumo wa hisa badala ya fedha taslimu, hivyo kila mwanahisa atapewa hisa za ziada kwa thamani halisi ya gawio analostahili kupewa. Maamuzi haya yalifikiwa ili kuiwezesha benki kuimarisha zaidi mtaji wake hasa kipindi hiki ambapo imepata kibali cha kutanuka na kufanya kazi nchi nzima,” amesema.

Kaimu mkurugenzi huyo amesema utoaji mikopo umeongezeka kutoka Sh61 bilioni mwaka 2022 hadi kufikia Sh74 bilioni mwaka 2023 huku amana za wateja zikiongezeka kutoka Sh78 bilioni hadi Sh90 bilioni.

Tarimo amesema benki hiyo imeendelea kuwekeza kwenye teknolojia na sasa iko katika hatua za mwisho kuanzisha huduma mpya za kidijitali zitakazoiwezesha kuongeza faida.

Meneja Usajili wa Hisa na Hati Fungani kutoka Kampuni ya Uhifadhi wa Dhamana zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (CSDR), Gideon Kapange, amesema kulingana na taratibu za soko hilo hisa zitaanza kuuzwa kwa siku 14 na mtu yeyote akinunua ndani ya kipindi hicho atastahili kulipwa gawio.

Related Posts