Morogoro. Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha moto ulioteketeza vibanda tisa katika kituo cha mabasi Msamvu ni jiko la mkaa lililoachwa linawaka kwenye kibanda cha mama lishe.
Marugujo ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Julai 24, 2024 kwa waandishi wa habari, akisema mama lishe huyo baada ya kumaliza shughuli zake, alifunga kibanda na kuacha jiko hilo likiwa na moto.
Hata hivyo, amesema bado wanaendelea kuchunguza kujua namna moto huo ulivyosambaa na kushika vibanda vingine.
“Baada ya kufanikiwa kuuzima, kazi iliyofuata ni sisi kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kufanya uchunguzi kujua chanzo.”
“Tuliwahoji mashuhuda na wafanyabiashara wachache ambao waliofika usiku ule na pia tulikagua eneo la tukio, ndipo tukakuta kibanda cha mama lishe nyuma ya vile vibanda vya stendi, tukagundua kulikuwa na jiko lililoachwa linawaka,” amesema Kamanda Marugujo.
Amesema taarifa walizozipata, zinasema mama lishe huyo amekuwa akipika supu asubuhi na chakula cha mchana, na anapomaliza biashara zake huondoka na kuacha majiko na vitu vingine kwenye kibanda hicho.
Kamanda Marugujo amesema pamoja na kupata taarifa za awali, bado kikosi hicho kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kinaendelea kufanyia kazi taarifa za mashuhuda na wafanyabiashara, kujua kama kuna chanzo tofauti cha moto huo.
Pia amewataka mama na baba lishe katika eneo la Stendi ya Msamvu na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, kuacha tabia ya kufungia majiko ndani yakiwa na moto.
Amesema kufanya hivyo ni hatari kwa usalama wa mali zao na hata mali za wengine waliopo jirani.
Hata hivyo, Marugujo amewataka wafanyabiashara kufuata taratibu katika kuunganisha umeme kwenye vibanda, akisema kinyume chake kinaweza kuwa chanzo cha ajali za moto.
“Unakuta mfanyabiashara amejiunganishia umeme kutoka kibanda cha jirani bila kufuata utaratibu na hata vifaa anavyotumia kuunganisha ni vile ambavyo havina ubora. Hii ni hatari, ni vema wafanyabiashara wakafuata taratibu kupitia Tanesco ili kuepuka matukio kama haya,” amesema Kamanda Marugujo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema hasara iliyotokana na moto huo haijafahamika, wanaendelea kukusanya taarifa za wafanyabiashara walioathirika na ajali hiyo.
“Ajali ile ya moto ilitokea usiku, asubuhi hii tunaendelea na kukusanya taarifa za wafanyabiashara wote walioathirika kwa lengo la kueleza umma ni hasara kiasi gani imetokana na ajali hii,” amesema Kamanda Mkama.