Kamala Harris abadilisha upepo wa Trump

Mara baada ya mdahalo kati ya Donald Trump mgombea urais wa Republican na Rais Joe Biden wa chama Marekani cha Democrat na jaribio la mauaji ya Trump, ilionekana dhahiri chama cha Democrat kilianza kuelemewa kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba 2024.

Hata hivyo, kitendo cha Rais Biden kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumpendekeza makamu wake, Kamala Harris kugombea kiti hicho, kimebadilisha upepo wa kisiasa, hususan baada ya Kamala kuhutubia jana Jumanne Julai 2024.

Kamala alifanya mkutano wake wa kwanza wa kampeni huko Wisconsin jana Jumanne baada ya Rais Biden kuachana na azma ya kugombea tena kiti hicho.

Wakati wa hotuba yake huko Wisconsin, mgombea huyo mpya wa Democrat mwenye umri wa miaka 59, alimtuhumu mpinzani wake Trump kuwa anataka “kurudisha nchi yetu nyuma.”

“Tunataka kuishi katika nchi yenye uhuru, huruma na utawala wa sheria, au nchi ya machafuko, hofu na chuki?” aliwauliza waliohudhuria.

Kamala amemshambulia Trump katika mkutano huo wa kwanza wa kampeni yake ya kuelekea Ikulu, akionyesha uchaguzi wa Novemba 2024 ni kati ya mwendesha mashtaka wa zamani na mhalifu aliyepatikana na hatia.

Alirudia maoni yake ya Jumatatu, ambapo alikumbuka wakati wake kama mwendesha mashtaka huko California.

Akizungumza na umati wa watu wapatao 3,000 katika jimbo la Wisconsin, Kamala alimfananisha mpinzani na matapeli ambao alisema amewashtaki.

“Nilipambana na wahalifu wa aina zote,” amesema na kuongeza: “Wanyanyasaji waliokandamiza wanawake. Matapeli waliolaghai walaji. Wadanganyifu waliovunja sheria kwa faida yao binafsi… hivyo nisikilizeni ninaposema najua watu aina ya Donald Trump… katika kampeni hii, nawaahidi, nitaweka rekodi yangu dhidi yake siku yoyote ya juma.”

Kamala pia alimkosoa Trump kuhusu suala la utoaji mimba, akisema Rais wa zamani kupitia chama cha Republican anaunga mkono marufuku ya utoaji mimba kitaifa.

“Tunawaamini wanawake, na tunaheshimu uamuzi wao kuhusu miili yao wenyewe na si kuwa na serikali ya kuwaambia cha kufanya,” alisema Kamala.

Mahakama Kuu ya Marekani yenye wingi wa wahafidhina ilipindua uamuzi wa kihistoria wa Roe v. Wade mwaka 2022, ambao ulisema Katiba ya Marekani kwa ujumla inalinda haki ya mwanamke kutoa mimba. Tangu hukumu ya Roe v. Wade ilipopinduliwa, suala la utoaji mimba limewekwa mbele katika siasa za Marekani.

Roe v. Wade ilikuwa na kesi muhimu katika historia ya sheria ya Marekani, iliyokubaliana na haki ya kikatiba ya mwanamke kufanya uamuzi wa kutoa mimba.

Kufuatia maneno ya Kamala dhidi ya Trump, umati ulipiga kelele “Kamala! Kamala!” Watazamaji wengine walibaini kwamba shauku ya hadhira ililingana na ile iliyoonekana katika matukio ya Biden kwenye kipindi cha uchaguzi uliopita.

Jina la Trump lilipotajwa kwenye mkutano huo, sehemu kubwa ya umati walipiga kelele “mfungeni” wakikumbusha kauli kama hiyo iliyotolewa katika matukio ya Trump alipokuwa akishindana na Hillary Clinton mwaka 2016.

Wakati huohuo, Trump alichapisha kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii, Truth Social, kwamba Kamala ndiye makamu wa rais asiye na umaarufu zaidi katika historia ya Marekani.

Kampeni ya Harris imekusanya zaidi ya dola milioni 100 (zaidi ya Sh260 bilioni) ndani ya saa 36 baada ya Biden kujiondoa.

Kwa kuongezea hilo, kura mpya ya maoni iliyofanywa na Reuters na Ipsos imeonesha Kamala anaongoza kwa alama mbili dhidi ya Trump, asilimia 44 dhidi ya asilimia 42.

Pengine muhimu zaidi, Kamala ameungwa mkono na Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi, ambaye ni muhimu kwenye kampeni za Kamala.

Baada ya Pelosi kusema anamuunga mkono Kamala “rasmi, binafsi na kisiasa,” viongozi wengine wa bunge walifuata mkondo huo.

Hadi juzi Jumatatu jioni, Kamala alikuwa ameungwa mkono na zaidi ya wajumbe wa kutosha, 1,976, atakaowahitaji ili kushinda uteuzi kwenye kura ya kwanza.

Mchuano wa kisiasa kati ya Trump na Kamala kuelekea uchaguzi wa Novemba 2024 utaathiriwa na vipengele vingi muhimu vya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Trump ni kiongozi maarufu ndani ya chama cha Republican. Ana wafuasi wengi wanaomwona kama kiongozi mkweli na mwenye nguvu. Ana uzoefu wa kuwa rais wa Marekani (2017-2021) na anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama chake.

Hata hivyo, anakumbwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kesi na upinzani mkali kutoka kwa Democrats na baadhi ya wafuasi wa Republicans.

Kwa upande mwingine, Kamala kama makamu wa rais ana uzoefu wa utawala wa juu serikalini. Ni mwanamke wa kwanza mweusi kushika nafasi hiyo, jambo linalompa mvuto wa kipekee kwa wapiga kura wa makundi mbalimbali.

Hata hivyo, anakabiliwa na changamoto za kushawishi wapiga kura kuwa ana uwezo wa kuongoza nchi kwa ufanisi kutokana na ukosoaji wa utendaji wake kama makamu wa rais.

Trump anaendelea kusisitiza sera za ‘Marekani Kwanza,’ ambazo ni pamoja na kupunguza uhamiaji, kuongeza ushindani wa kiuchumi wa Marekani na kuimarisha jeshi. Anaunga mkono sera za kupunguza kodi na kupunguza ukali wa kanuni za kibiashara, na pia ana msimamo mkali kuhusu China na biashara ya kimataifa.

Pia Harris anasisitiza ajenda zinazolenga usawa wa kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, haki za kijamii na kuboresha elimu. Anaunga mkono sera za mazingira na anapigia debe juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Harris pia anataka kuimarisha haki za wafanyakazi na kuboresha sheria za uhamiaji.

Trump ana ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na amekuwa na uwezo wa kutumia majukwaa haya kueneza ujumbe wake moja kwa moja kwa wafuasi wake. Hata hivyo, akaunti zake zilifungiwa kwenye baadhi ya majukwaa makubwa kama Twitter, lakini anaweza kutumia njia mbadala kama vile Truth Social ambayo anaitumia kwa sasa.

Kwa upande mwingine, Kamala anaweza kufaidika na ushawishi wa vyombo vya habari vya jadi na mitandao ya kijamii. Anahitaji kujenga taswira ya kiongozi mwenye uwezo wa kushughulikia changamoto kubwa zinazokabili Marekani.

Trump anajulikana kwa msimamo wake wa kuboresha uchumi kupitia sera za kupunguza kodi na kupunguza vizuizi vya kibiashara. Ataendelea kutumia hoja ya mafanikio ya kiuchumi ya kipindi chake cha kwanza kama rais kama kivutio kwa wapiga kura.

Lakini Kamala atasisitiza kuboresha usawa wa kiuchumi na kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini na cha kati. Anaweza kupata ushawishi mkubwa ikiwa ataweza kushawishi wapiga kura kuwa sera zake zitaleta maendeleo ya kiuchumi kwa wote, sio tu kwa matajiri pakee.

Hata hivyo, kujitokeza kwa Kamala baada ya kujitoa kwa Rais Biden kumerejesha nguvu kwenye kampeni ya uchaguzi wa Marekani ambayo ilikuwa imeshindwa kuwavutia wapiga kura ambao walikuwa wanalazimika kuchagua kati ya Biden na Trump, pamoja na hali ya uchumi, sera za kigeni za Marekani na masuala mengine.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts