WIKI iliyopita wakazi wa San Marino, nchi ndogo iliyozungukwa na milima kaskazini mwa Italia walifanya tamasha la kufurahia kupanda daraja katika viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (Fifa).
Nchi hiyo yenye ukubwa wa kilomita 6.2 za mraba ikiwa na watu 34,000 ambayo siku zote huwa na watalii wasiopungua 10,000 ilipanda daraja kutoka nafasi ya 208 ya wanachama wa Fifa na kuwa ya 207 kutokana na Eritrea iliyokuwa juu yao mkiani kufutwa uanachama na Fifa.
Kocha wa timu ya taifa ya San Marino, Franco Verrella alisema japokuwa kupanda daraja ni tofauti, lakini wananchi wanasubiri ushindi wao wa pili. Tangu mwishoni mwa mchezo wao dhidi ya Malta, San Marino wamecheza michezo 137 na waliwahi kuwa mbele katika umiliki wa mpira kwa dakika sita tu mara ya kwanza dhidi ya wapinzani wao hao Agosti 2012.
Pamoja na hayo, lakini Wasanmarino watafurahi zaidi kuona kwamba kuna mwanachama mwingine wa Fifa anaondolewa ili wapande zaidi kwa viwango, japokuwa wataendelea kushika mkia.
Siku zote yakifanyika mashindano ya kimataifa ya soka ya kufuzu kwa ajili fainali za Ulaya au Kombe la Dunia kinachoulizwa ni San Marino wataondoka uwanjani na kapu cha mabao mangapi?
Bahati mbaya vyombo vya habari havitoi taarifa za michezo za nchi hiyo na Watanzania wengi wakiwemo waandishi wa habari hawajui hata nchi hiyo ipo wapi.
Mara ya mwisho kwa timu ya nchi hiyo kupata ushindi ilikuwa Aprili 28, 2004 kwa kuifunga Liechtenstein ambayo inapakana na Uswisi upande wa Magharibi na Austria iliyopo Kusini.
Mpaka leo watu za San Morino wanasubiri kipenga cha mwisho kikipulizwa wawe ndio washindi katika mchezo wowote wa soka ambao timu yao ya taifa itacheza. Na mpaka sasa wamecheza michezo zaidi ya 200, lakini hawajashinda hata mara moja.
Nchi hiyo ni moja ya jamhuri kongwe duniani (ikiwa na miaka 1,700), lakini haitajiki sana na kinachojulikana na wengi ni utaalamu wa watu wake katika ujenzi wa makasri na majengo ya kihistoria ya karne ya 11, ufinyanzi na uchongaji wa miamba ya mawe.
San Morino haina jeshi, bali ina askari wachache na gereza lipo tupu baada ya mfungwa pekee kumaliza adhabu ya kukaa jela mwaka uliopita. Huyo mfungwa wakati alipokuwa akitumikia adhabu ya miezi minane aliwahi kulalamika kuwa
maisha ya upweke gerezani ni mateso na aliiomba serikali impatie mfungwa mwingine wa kuzungumza naye mara kwa mara kwa vile amechoka kuangalia runinga na kuzungumza na watu kwa simu.
Kila siku alikuwa anatolewa kwenda kutembea mjini kwa saa moja na kila aliporudi alikuta chakula chake kilichoagizwa kutoka hoteli kinamsubiri. Hapo gerezani ipo maktaba na chumba cha mazoezi.
Watu wa nchi hiyo wanapenda michezo, lakini katika soka wamegeuzwa kama zulia, kila anayepewa analikung’uta vumbi sawasawa. Nchi hiyo ina klabu za soka 15 na klabu moja, San Marino Alcio inashiriki katika ligi ya Itaia ya daraja la nne.
Uwanja wake mkubwa wa mpira unaochukua watazamaji 7,000 ulifunguliwa 1991. Kwa kawaida unapochezo mchezo wa kimataifa watu waliotoka nchi jirani huwa zaidi ya nusu ya watazamaji.
Tangu mwaka 1990 San Marino imeshiriki katika mashindano ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) na kufuzu Kombe la Dunia, lakini haijawahi kushinda hata mchezo mmoja.
Mchezo pekee ambao nchi hiy imeshinda ni ule wa kirafiki na nchi ya Liechesten (nchi ndogo ambayo ipo Ulaya) uliopigwa Aprili 28, 2004.
San Marino siku zote imekuwa katika nafasi za mwisho na hasa kushika mkia katika viwango Fifa na mara moja mwaka 2008 ilikuwa ya pili kutoka mkiani ambapo ilikuwa pamoja na Bhutan.
Kwa mshangao wa wengi ilitoka sare bila ya kufungana na Estonia katika mashindano ya Euro 2016 na ilifunga bao lake la kwanza nje ya nchi ilipocheza na Lithuania miaka 18 iliyopita.
Katika kushiriki kwake kwa mara ya kwanza Kombe la
Dunia miaka 20 iliyopita iliwekwa katika kundi moja na England, Uholanzi, Norway na Uturuki.
Katika mchezo wa kwanza ilichapwa 10-0 na Norway, lakini ziliporudiana ikalala 2-0. Uturuki iliifunga 4-1 katika mchezo wa kwanza na kufanikiwa kwenda suluhu katika mchezo wa marudiano.
Machi 10, 1993, San Marino ilipokutana na England iliweka historia ya kufunga bao la pili la haraka katika historia ya Kombe la Dunia. Bao hilo lilifungwa sekunde ya 8.3 baada ya mchezo kuanza, lakini filimbi ya mwisho ilipopulizwa San Marino ilikuwa imechapwa 7–1.
San Marino ilimaliza michezo yake 10 katika kundi hilo ikibugia mabao 46.
Katika michezo ya mtoano ya mashindano ya Euro 2004, San Marino ilifungwa katika michezo yote minane na haikufunga hata bao moja. Matokeo yao mazuri kabisa katika mashindano hayo yalikuwa kufungwa mabao 10 na Latvia dakika moja kabla ya mchezo kumalizika. Baaada ya mchezo huo kocha wa Latvia, Gary Jhnson alijiuzulu.
Katika mchezo wao wa kwanza wa makundi katika Euro 2008 San Marino ilifungwa nyumbani kwa mabao 13-0 na Ujerumani.
San Marino katika mashindano hayo walifungwa jumla ya mabao 57 na wao kufunga mabao matatu – moja katika kila mchezo walipocheza na Ireland, Cyprus na Wales.
Nchi hiyo ilikuwa na matokeo mabaya pia katika michezo ya makundi ya kuwania tiketi za fainali za mwaka 2010 za Kombe la Dunia. Ilipoteza michezo yote kwa kupachikwa mabao ikiwa ni pamoja na kufungwa mabao 10-0 na Poland.
Katika michezo yote hiyo ilifanikiwa kufunga bao moja pale ilipocheza na Slovakia na kufungwa mabao 3-1. Matokeo mabaya kabisa yalikuwa ya kufungwa mabao 11-0 na Uholanzi na mazuri ni kufungwa bao 1-0 na Finland.
Novemba 15, 2014 watu wa San Marino walikuwa na sherehe kubwa kufuatia kwenda suluhu na Estonia. Hiyo ilikuwa
mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10 ya kushiriki michezo ya kimataifa na kumaliza mchezo wakiwa hawajafungwa.
Karibu wachezaji wote wa timu ya taifa ya nchi hiyo ni wauza maduka, madereva na makondakta wa mabasi, vijana wanaotembeza watalii pamoja na wafanyakazi wa serikali na kampuni. Kocha wao ni seremala.