Magari Dar, Arusha upinzani umerudi upyaa

USHINDI wa 1-2-3 walioupata madereva wa timu ya Mitsubishi dhidi ya madereva wa Subaru, siyo tu umefufua upinzani wa timu hizo, bali pia na ule uliodumu miaka mingi kati ya klabu za Arusha na Dar es Salaam.

Yakijinadi kwa jina la Advent Rally of Tanga, mashindano ya mbio za magari ya kufungua msimu yalimalizika mjini Tanga kwa timu ya Mitsubishi kuondoka na pointi 58 wakati Subaru ikiondoka na pointi 22.

Alyevuna pointi nyingi kuliko wote ni Randeep Birdi aliyezoa 25 kwa kumaliza wa kwanza katika mashindano akiendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 1X na kufuatiwa na dereva kutoka Arusha Gurpal Sandhu aliyeondoka na pointi 18 baada ya kumaliza wa pili akiwa na Mitsubishi Evo X.

Ushindi wa 1-2-3 kwa Mitsubishi ulihitimishwa na Manveer Singh wa Dar es Salaam aliyepata pointi 15 baada ya kumaliza wa tatu akitumia pia Mitsubishi Evo 1X.

Aliyeleta pointi kwa timu ya Subaru Impreza alikuwa Yusuf  Akida wa Tanga aliyetengeneza pointi 12 kwa timu yake na mkoa wake baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu.

Pointi 10 kwa timu ya Subaru Impreza zilipatikana kupitia Vishal Patel wa Dar es Salaam aliyemaliza nafasi ya tano.

Wakati ushindani kati ya Mitsubishi na Subaru ukifikisha miongo miwili sasa, upinzani kati ya madereva wa Dar es Salaam na Arusha pia unagonga mwaka wa 20 hivi leo.

Dereva anayeongoza mbio hizo Randeep Birdi wa Dar es Salaam na mpinzani wake wa karibu, Gurpal Sandhu wa Arusha wamekuwa wakipokezana taji la ubingwa wa mbio za magari kwa takriban miaka 10.

“Gari yangu ilipata hitilifu kidogo katika hatua mbili za awali, lakini nikaweza kufanya vizuri katika hatua ya tatu, nne na ya tano na hivyo kufanikiwa kumshinda mpinzani wangu wa karibu kwa zaidi ya dakika moja,” alisema Birdi ambaye ameshinda taji la ubingwa wa taifa mara nyingi katika miaka 18 ya ushiriki wake.

Madereva wengine walioshinda mbio za magari kwa miaka ya karibuni ni Kirit Pandya, Dharam Pandya, Mohamed Tufail Amin na Jamil Khan wa Dar es Salaam, wakati kutoka Iringa  ni Ahmed Huwel. Kabla ya Gurpal Sandhu, Mkoa wa Arusha ulichukua ubingwa wa taifa kupitia kwa Navraj Hans, Amarjeet Dhillon Sunvic na Gerald Miller.

Akiwa nyuma ya Birdi kwa pointi saba, Sandhu anaupa Mkoa wa Arusha nafasi ya pili nyuma ya Dar es Salaam katika mbio za ubingwa huku zikiwa zimebaki raundi nne  kumalizika kwa msimu Desemba, mwaka huu.

Related Posts