Steven Mashishanga ni kati ya wanasisasa wakongwe nchini ambao watakumbukwa kwa mchango wao katika utumishi wa umma, hasa katika nafasi ya mkuu wa mkoa aliyoitumikia wakati wa Serikali ya awamu ya tatu chini ya Hayati Benjamin Mkapa.
Amefanya kazi kama mkuu wa mkoa kwenye mikoa tofauti, ikiwamo ya Tabora (1995 – 1999), Mwanza (1999 – 2003) na Morogoro (2003 – 2006) kabla ya kustaafu utumishi wa umma akiwa na umri wa miaka 72.
Mwanasiasa huyo mkongwe alipata umaarufu zaidi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Licha ya kuwa mzaliwa wa Shinyanga, aliamua kuweka makazi yake Morogoro kwa kuwa aliupenda mkoa huo kwa maelezo yake.
Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Mashishanga ambaye Julai 27, mwaka huu anatimiza miaka 90, na katika mahojiano hayo, amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwamo namna alivyopambana na migogoro baina ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro.
Morogoro ni moja ya mikoa inayoongoza nchini kwa migogoro ya ardhi, ambayo kwa sehemu kubwa inahusisha wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakigombana hadi kuuana kwa sababu ya ardhi.
Alivyoshughulikia migogoro
Mashishanga anaeleza kwamba alipelekwa Mkoa wa Morogoro na Rais Mkapa kwa mambo makuu mawili; migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na elimu ambayo wakati huo Morogoro haikuwa vizuri.
Anasema wakati akiwa mkuu wa mkoa, alitumia muda wake mwingi kwenye ziara kukutana na wananchi ambapo alikuwa akiambatana na maofisa wake ili kutatua migogoro na hiyo iliwasaidia kuipunguza.
“Wakati wa uongozi wangu nilikua nafanya ziara za kushtukiza kwa kila wilaya na katika kila ziara yangu niliambatana na mwanasheria na migogoro mingi tuliweza kuitatua. Sikuwa nakaa ofisini, hii ilinisaidia kujua changamoto za wananchi, hasa vijijini.
“Katika kipindi changu, hakuna mtu aliyeathirika kimaisha kwa migogoro ya wakulima na wafugaji,” anaeleza Mashishanga, wakati wa mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake, Morogoro.
Hata hivyo, anabainisha kwamba uamuzi wa Serikali kuruhusu wafugaji kutafuta malisho, ulichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la migogoro ambayo hadi sasa inaendelea kuwaathiri wananchi katika mkoa huo.
Anasema kwa sasa migogoro hiyo imepungua kutokana na jitihada za Serikali za kuitatua, hivyo anashauri kuwepo kwa mikakati mahsusi ya kushughulikia changamoto hiyo kwa maeneo yote yenye migogoro.
“Kwa sasa migogoro inapungua kwa sababu viongozi waliopo sasa wanahangaika kuhakikisha watu hawaingii tena kutoka maeneo mengine na kuja hapa Morogoro, lakini Serikali ina mpango wa kujenga mabwawa ili kukomesha migororo kati ya wakulima na wafugaji,” anasema Masishanga.
Mashishanga anasema sekta ya kilimo ndiyo mkombozi wa uchumi wa Tanzania na Mkoa wa Morogoro unafanya vizuri kwenye eneo hilo, hata hivyo, anashauri kufanyika kwa kilimo cha kisasa ili kuongeza mapato.
“Kilimo cha kisasa ndiyo suluhu ya changamoto hii, Serikali inafanya kazi kubwa kuboresha miundombinu, naomba wananchi waitunze. Mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (Bulding a Better Tomorrow) ni jambo jema ambalo litainua uchumi wa vijana na taifa kwa ujumla.
“Ile mito inayopita kila kijiji, kila kata, yangewekwa mabwawa mengi, Morogoro ingekuwa inazalisha chakula cha kutosha na ingeuza sana nje ya nchi na uzalishaji wa chakula ungekuwa mkubwa ukilinganisha na sasa,” anasema.
Anaongeza kuwa Ilani ya CCM katika mwongozo wake wa 81, inazungumzia habari ya kuwaletea watu huduma ya maji ili walime kilimo cha umwagiliaji, kwa sasa Morogoro inazalisha chakula kidogo”.
Akiwa mmoja wa wastaafu nchini, Mashishanga anasema anafarijika kuona anathaminiwa na jambo hilo limemfanya aendelee kuwa na afya njema licha ya kuwa na umri mkubwa. Anasema hana tatizo na mtu yeyote.
“Kwa upande wangu, nakiri wazi kwamba ninathaminiwa na ndio maana mnaniona nina afya njema, unadhani tunatengwa, hapana, lakini sifahamu kwa upande wa wenzangu wengine.
“Mimi sina tatizo na mtu yeyote kuanzia uogozi wa kijiji na pia ninaheshimiwa sana siyo tu na viongozi hadi, na wananchi pia.
“Viongozi wanapopita hapa Morogoro, wanakuja kunijulia hali na pia serikalini kwenye vikao vya manispaa naitwa kama mzee mstaafu.
“Naheshimika sana, sijui wenzangu huko waliko lakini mimi nipo very comfortable (nimeridhika),” amesema Mashishanga.
Anawataka Watanzania kuzingatia umoja wa kitaifa na wasiruhusu kugawanywa na watu wenye tamaa ya rasilimali ambao wanaleta vitendo vya ukiukaji wa maadili. Amewataka washirikiane kukemea hilo ili rasilimali zilizopo zibaki nchini.
“Wanaotumwa kuja huku wanataka tugombane na tukigombana vita itakuwa kubwa sana, nani ataweza kupigana na Marekani? Na wanaomtukana Rais wetu, ikiibuka vita wanapanda ndege kwenda nje haraka sana,” anasema Mashishanga.
Mashishanga ambaye alizaliwa Julai 27, 1934, anafikisha umri wa miaka 90 na mwaka huu, anasema atakwenda nyumbani kwao Shinyanga kwa ajili ya sherehe hiyo ya kuzaliwa. Siri kubwa anasema ni kutunzwa na watoto wake na pia hanywi pombe.
“Ni kweli Julai 27, mwaka huu, ninategemea kufikisha miaka 90. Mwaka jana nilifanyia sherehe yangu ya kuzaliwa Morogoro, mwaka juzi Shinyanga na mwaka huu nitarudi tena nyumbani Shinyanga. Familia yangu na watoto wangu wanasaidia kuhakikisha kuwa nina afya imara, lakini pia niseme ni uwezo wa Mungu mimi kuishi hadi sasa.
“Mwaka 2014 nilifiwa na mke wangu, kama familia yangu ingeniacha sasa hivi ningekuwa nimefariki, lakini wanahakikisha ninakula vizuri na ninapata mahitaji yote muhimu.
“Vilevile, mimi pia ni muumini wa dini ya Kikristu, naenda kanisani na sinywi pombe.
“Niliacha kunywa pombe tangu nilipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro hadi leo na pia niliishi na watu vizuri bila kuwabagua, nafikiri hayo ndiyo yanasababisha niishi hadi sasa,” anasema Mashishanga.
Kuhusu kuamua kuishi Morogoro, Mashishanga anasema kilichomvutia kubaki katika mkoa huo ni kwa kuwa umejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na mazao mengi, yanastawi kila wilaya na una mito mingi, wakati ule akiwa mkuu wa mikoa ilikuwepo mito 130.
“Fursa hii ya kilimo cha umwagiliaji ilinivutia zaidi kuweka makazi Morogoro, ni tofauti na kule kwetu Maswa, Shinyanga, mvua ikikauka hakuna maji kama huku. Ningerudi kule lakini nikaona nibaki hapa nifanye kilimo,” anasema Mashishanga.
Mwanasiasa huyo anaeleza kwamba Rais Samia amekuwa kiongozi bora kutokana na kazi kubwa anayofanya ya kuleta maendeleo. Amewataka Watanzania wamuunge mkono ili aendelee kufanya kazi yake vizuri.
“Kwanza kabisa nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchapa kazi na kuifungua nchi, anafanya kazi kubwa, hivi karibuni tumeshuhudia reli ya kisasa (SGR) ikianza kufanya kazi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, haya ni mafanikio makubwa sana. Nina shauku kubwa nikapande SGR.
“Tumsapoti Mama, halali. Kuna watu wanamtukana na bado wanaenda kwenye nyumba za ibada, unaenda kufanya nini, niwaombe viongozi wa dini wakemee suala hilo kwa nguvu, kuna watu wanasubiri tugombane ili waje wachukue vitu tulivonavyo,” anasema.