JINA la Ley Matampi ni kati ya 32 ya kikosi cha Coastal Union kitakachoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Matampi ambaye alikuwa anatajwa kuondoka kikosini kwa madai kuwa hana mkataba na timu hiyo amerejea nchini na kujiunga na wenzake tayari kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na mashindano mengine.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub, amesema Matambi amerejea na amejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 32 ambao wamesajiliwa dirisha la usajili wa CAF kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Kawasili juzi akitokea nchini kwao na jana alipanda boti kujiunga na wachezaji wenzake ambao wapo Pemba kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na michuano mingine ya ndani na kimataifa,” amesema.
“Ley Matampi ni mchezaji wetu na mkataba wake bado upo. Kuchelewa kujiunga na kambi sio sababu kwamba alikuwa na mgomo, hapana, alikuwa na ruhusa binafsi na uongozi ulikuwa unatambua hilo. Juu ya kumaliza mkataba sidhani kama angeweza kurejea.”
Pia alitumia nafasi hiyo kutamba kuwa mkali wa klinshiti ametua na kuwataka mashabiki wa Coastal Union na soka wakutane katika Ngao ya Jamii.
Matampi ambaye aliongoza kwa kuwa na klinshiti 15 msimu ulioisha akimzidi kipa bora wa mara mbili mfululizo, Djigui Diarra amerejea na anaanza mazoezi na wenzake leo.
Kipa huyo ameiwezesha Coastal Union kumaliza nafasi ya nne msimu huu na kupata katika nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa, michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika alijiunga na timu hiyo akiwa mchezaji huru baada ya kumalizana na waajiri wake FC Lupopo ya Congo.