Mdogo wa Hans Poppe, mwanawe wajisalimisha mahakamani

Hatimaye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Z.H.Poppe Limited, Caeser Hans Poppe na mwanawe Adam Caeser Hans Poppe, wamejisalimisha wenyewe Mahakama Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC Temeke).

Hatua hiyo ya Caeser na Adam kujisalimisha wenyewe, Mahakamani hapo bila kukamatwa, inatokana na Mahakama hiyo kutoa amri ya kukamatwa kwa wakurugenzi hao kwa kosa la kuidharau.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya Caeser na  Adam kushindwa kufika mahakamani hapo kutoa orodha ya mali iliyokusanywa na kampuni hiyo pamoja na nyingine, katika kesi ya mirathi ya namba 177/2022 ya marehemu Zacharia Hans Poppe.

Julai 5, 2024 Mahakama hiyo ilielekeza Caeser na Adam wakamatwe na wapelekwe mahakamani hapo ili washtakiwe kwa kosa la kuidharau Mahakama.

Caeser ni mdogo wake Zacharia Hans Poppe ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, alitakiwa afike mahakamani hapo siku hiyo na mwanawe, lakini hakufanya hivyo na ndipo Mahakama ilipotumia mamlaka yake hayo.

Caeser na Adam ni wakurugenzi wenza wa kampuni za marehemu Zacharia Hans Poppe, walitakiwa kufika kwa ajili ya kueleza hali ya mali za marehemu Zacharia zilizopo katika kampuni zake ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi, lakini hawakutokea siku hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Glady’s Nancy Barthy alitoa amri ya kukamatwa kwa watu hao baada ya kushindwa kufika tarehe hiyo iliyopangwa.

Hata hivyo leo, Caeser na Adam walifika mahakamani hapo na kuomba Mahakama isitekeleze amri ya kuwashtaki kama ilivyokuwa imeelekeza kwa sababu wametii amri ya kwenda  wenyewe mahakamani.

Wakurugenzi hao kupitia wakili wao kutoka kampuni ya Tan Law Africa, Peter Kibatala akisaidiana na Alphonce Nachipiangu, Gloria Ulomi na Rebecca Lyaka waliomba Mahakama hiyo iondoe amri iliyokuwa imetoa mwanzoni mwa mwezi huu ya kuwakamata na isitekeleze amri iliyokuwa imeelekeza ya kuwashtakiwa kwa sababu wamefika wenyewe bila kukamatwa. 

Jaji Barthy anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na ombi la Kibatala na kuondoa amri ya kuwakamata na kuelekeza tarehe itakayopangwa na Mahakama hiyo wakurugenzi hao pamoja na wasimamizi wa mirathi wafike siku hiyo  mahakamani hapo bila kukosa.

“Naelekeza wakurungenzi hawa na wasimamizi wa mirathi tarehe itakayopangwa na Mahakama hii mnatakiwa mfike bila kukosa,” alisema Jaji Barthy. Pia Mahakama imeelekeza wasimamizi wa mirathi nao wanatakiwa siku hiyo wafike mahakamani Agosti 20, 2024.

Awali, shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kujua iwapo amri iliyotolewa na Mahakama imefanyiwa kazi ya kukamatwa kwa Caeser na Adam.

Chimbuko la wakurugenzi hao kuitwa mahakamani linatokana na watoto wa marehemu Zacharia, Angel na Abel ambao ni wasimamizi wa mirathi ya baba yao kuiomba Mahakama hiyo iamuru na iwaite ili waje watoe taarifa ya fedha ikiwemo mapato na matumizi yaliyopo katika kampuni ya baba yao mzazi iitwayo Z.H.Poppe Ltd ambayo kwa sasa inasimamiwa na Caeser na Adam.

Katika maombi hayo Wakili Regina Helman anayemwakilisha mtoto mkubwa wa marehemu Zacharia, Analisa Zacharia Hans Poppe aliiomba Mahakama hiyo Caeser na Adam waitwe mahakamani hapo kwa sababu wao ndio walioshikilia hisa na mali za Zacharia katika kampuni zake na pia wanadaiwa kuendesha kampuni hiyo bila kuwashirikisha warithi ambao ni watoto.

Ombi hilo la kukamatwa kwa wakurugenzi hao liliungwa mkono na wakili Emmanuel Msengezi anayewatetea wasimamizi wawili wa mirathi ya Zacharia ambao ni Angel Zacharia Hans Poppe na Abel Zacharia Hans Poppe.

Msengezi alidai katika kampuni hizo, Zacharia Hans Poppe anamiliki hisa asilimia 90 wakati Caeser ana asilimia 10.

Zacharia Hans Poppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.

Hans Poppe anakumbukwa na wanachama wa Simba kwa kuiletea  mafanikio makubwa katika uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa pia kuwa mwenyekiti wa kundi la Marafiki wa Simba (Frienda of Simba) ambalo lilijizolea umaarufu mkubwa katika medani za soka hapa nchini.

Related Posts