Mkurugenzi ulinzi wa viongozi Marekani ajiuzulu sakata la Trump kupigwa risasi

Washington. Kufuatia jaribio la kumuua Rais wa zamani Donald Trump Julai 14, 2024, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ulinzi wa Viongozi (Secret Service) Marekani, Kimberly Cheatle, amejiuzulu huku uchunguzi ukiendelea kuhusu upungufu wa kiusalama uliojitokeza kwenye tukio hilo.

Katika tukio hilo, Thomas Matthew Crooks (20) alimfyatulia risasi Trump ambaye sasa ni mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Butler, Pennsylvania. Risasi moja ilimpiga Trump kwenye sikio, huku Crooks akiuawa kwa risasi muda huo huo, baada ya maofisa usalama kumwona. Baadhi ya watu walijeruhiwa.

Hatua hii inakuja wakati Bunge na maofisa wa serikali wakiendelea na uchunguzi juu ya jinsi shirika hilo lilivyoshughulikia ulinzi wa Trump na jinsi Crooks alivyojaribu kumuua. Cheatle amesema katika barua yake ya kujiuzulu kwamba amefanya uamuzi mgumu wa kuondoka kwenye shirika hilo kwa moyo mzito na kwamba hataki kuondoka kwake kuwakwaze wengine kutekeleza jukumu lao.

“Kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni, ni kwa moyo mzito kwamba nimefanya uamuzi mgumu wa kuachia nafasi yangu kama mkurugenzi wenu,” ameandika Cheatle. Amekubali kwamba Julai 13, siku ya tukio la risasi, shirika hilo lilishindwa kutimiza jukumu lake la kulinda viongozi wa taifa lao. Naibu mkurugenzi wa taasisi hiyo, Ronald Row, ameteuliwa kuongoza idara hiyo, Wizara ya Usalama wa Ndani imetangaza.

Katika taarifa yake, Rais Joe Biden amesema yeye na mkewe Jill Biden “wanashukuru” kwa muda wote ambao Cheatle ameitumikia taasisi hiyo. “Kama kiongozi, inahitaji heshima, ujasiri, na uadilifu mkubwa kuchukua jukumu kamili kwa shirika lililo na moja ya kazi ngumu zaidi katika huduma ya umma,” amesema Biden kuhusu Cheatle.

Kumekuwa na shinikizo kwa pande zote katika Bunge la Congress ya kutaka Cheatle ajiuzulu na msukumo kutoka kwa wabunge wa chama cha Republican kutaka aondolewe.

Wabunge walikuwa na hasira baada ya Cheatle kuonekana mbele ya Kamati ya Usimamizi ya Bunge Jumatatu, ambapo alikataa kujibu maswali mengi ya kamati hiyo. Wakati wa kuonekana kwake mbele ya Kamati ya Bunge, Cheatle alikubali kwamba kulikuwa na tatizo kubwa la usalama kwenye mkutano huo, lakini bado alikataa wito wa kujiuzulu.

“Nadhani mimi ndiye mtu bora kuongoza idara wakati huu,” alisema Cheatle Jumatatu. Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mike Johnson, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kujiuzulu kwa Cheatle kulichelewa.

\”Sasa tunapaswa kuanza upya.Tunapaswa kujenga upya imani na uaminifu wa Wamarekani kwa idara ya ulinzi wa viongozi. Ina jukumu muhimu sana la kulinda marais, marais wa zamani, na maofisa wengine wa dola, na tuna kazi nyingi ya kufanya,” amesema Johnson.

Cheatle aliteuliwa na Biden kuongoza idara hiyo mwaka 2022. Katika mahojiano na CNN wiki iliyopita, Cheatle alisema taasisi yake ilikuwa na jukumu pekee la kubuni na kutekeleza mipango ya usalama katika eneo la mkutano wa Pennsylvania, ambapo mtu mwenye bunduki alimpiga risasi Trump kutoka kwenye paa lisilolindwa, umbali wa futi chache kutoka jukwaa la mkutano.

Kumekuwa na maswali ya jinsi idara hiyo ilivyoshughulikia ulinzi wa Trump siku hiyo, ikiwa ni pamoja na kushindwa kudhibiti upatikanaji wa paa lisilolindwa na jinsi shirika lilivyoshughulikia taarifa kabla ya shambulio, ambazo zilimtambua mhalifu kama mtu aliyekuwa akifanya mambo ya kutiliwa shaka karibu na eneo la mkutano. Cheatle aliyeacha kazi ya kusimamia Usalama wa Kimataifa katika PepsiCo, amehudumu katika idara hiyo kwa miaka 27.

Related Posts